Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa Aprili 8, 2025 ulishiriki Jukwaa Maalum la Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi zinazozalisha Madini ya Almasi Barani Afrika (The African Diamond Producers Association – ADPA Council Of Ministers).
Mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Bintumani Mjini Freetown nchini Sierra Leone unatarajia kuhitimishwa Aprili 11, 2025 huku agenda mbalimbali zikitarajiwa kujadiliwa ikiwemo ya kupokea na kujadili taarifa ya mapato na matumizi ya fedha ya umoja huo pamoja na sera mpya ya uchangiaji wa ada kwa nchi wanachama.
Nchi zinazounda jumuiya hiyo zinahusisha nchi 21 ikiwamo Tanzania, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Namibia, Sierra Leone, Afrika ya Kusini, Togo na Zimbabwe.
Aidha, mbali na nchi wanachama, zipo pia nchi waangalizi ambazo jiolojia ya nchi husika zina uwezo wa kuzalisha madini hayo siku za usoni ambazo ni pamoja na Algeria, Mauritania , Ivory Coast, Liberia, Mali na Mauritania.
Mwaka 2022 wakati Tanzania ikiwa mwenyekiti wa umoja huo iliwezesha kupitiwa kwa mifumo kadhaa ya jumuiya hiyo ikiwemo Katiba, Kanuni na miongozo mbalimbali ambayo yote ililengakuhakikisha nchi wanachama zinanufaika na rasilimali hizo.

Katika kikao hicho nchi ya Sierra Leone ndiyo mwenyeji na ni Makamu Mwenyekiti. Kupitia Mkutano huu, Sierra Leone itakuwa Mwenyekiti baada ya Zimbabwe kumaliza kipindi chake.
Kwa mujibu wa Katiba, mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la umoja huo hudumu kwa kipindi cha miaka miwili.Wataalam wa Wizara ambao wamefuatana na Dkt. Kiruswa ni pamoja na mwakilishi wa Balozi nchini Nigeria, Allen Kuzilwa, Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia masuala ya wachimbaji wadogo Francis Mihayo na wataalam mhandisi Abeid Kidindi na Henry Shadolo.
More Stories
TMA yawataka wananchi kuzifanyia kazi taarifa inazotoa
TPDC, ZPDC zaendelea kushirikiana uendelezaji sekta ya gesi nchini
Nachingwea waanza kuona manufaa vituo vya kudhibiti wanyamapori waharibifu