November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yaomba kuisaidia Botswana kuimarisha upatikanaji wa Dawa

Na. Mwandishi wetu,Gaboron- Botswana

Tanzania kupitia Wizara ya Afya imewasilisha ombi kwa Waziri wa Afya wa Botswana Dkt. Edwin Dikolot la kusaidia nchi hiyo katika kuimarisha upatikanaji wa dawa.

Waziri wa Afya Tanzania Ummy Mwalimu amewasilisha ombi hilo leo Agosti 31, 2023 wakati wakijadiliana masuala ya upatikanaji wa dawa katika nchi hiyo ya Botswana.

“Nimewasilisha ombi kwa Waziri wa Afya wa Botswana Mhe Dkt. Edwin Dikolot la kutaka Tanzania iweze kuisaidia nchi hii katika kuimarisha upatikanaji wa dawa”, amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema kupitia ushirikiano uliopo kati ya Mammlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Tanzania na Mamlaka ya dawa ya Botswana (BoMRA) mktaba wa maelewano ulisainiwe kwa ajili ya kuipatia Botswana ushauri wa kitaalamu wa kuimarisha Tassisi yake.

Pia, Waziri Ummy amesema Tanzania inayo uzoefu wa kutosha katika ununuzi wa dawa ambapo imeingia mikataba na wazalishaji wakubwa wa dawa Duniani wapatao 233.

“Kupiti mfumo huu Tanzania inaweza kununua aina za dawa tofauti zipatazo 2209, Nchi yetu pia, imefanikiwa kupewa dhamana ya ununuzi wa dawa wa pamoja (Pooled Procurement) kwa nchi Mbili ambazo ni Commoro na Seychells ikiwamo Tanzania yenyewe”, amesema Waziri Ummy

Amesema, mpango huu ulifanikisha kupunguza gharama ya ununuzi wa dawa kwa asilimia 53 kwakuzingatia Azimio la SADC kwamba, Bohari ya dawa ya Tanzania isaidie nchi wanachama katika upatikanaji wa dawa.

Hata hivyo Waziri Ummy amemwomba Waziri Mwenzake Dkt. Dikolot kutumia Taasisi hii katika kuimarisha upatikanaji wa dawa Nchini Botswana.

Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Botswana, Dkt. Edwin Dikolot amemshukuru Waziri wa Afya Tanzania Ummy Mwalimu kwa kuleta wazo hili na akaelekeza Taasisi ya dawa ya Botswana kuanza mazungumzo na Bohari Kuu ya Dawa ya Tanzania.

“Kwanza nikushukuru sana Waziri Ummy kwa kuleta wazo hili kwetu na mimi naelekeza Taasisi ya dawa ya Botswana kuanza mazungumzo haraka na Bohari Kuu ya Dawa ya Tanzania kwa kuweka hati ya makubaliano na hatimaye kufanikisha utekelezaji wa makubaliano hayo”, amesema Dkt. Dikolot Waziri wa Afya Botswana