Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAZIRI wa Nishati, Dkt. Juma Homera, amesema Tanzania imejipanga kutumia fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati duniani kwa kuvutia mitaji ya ndani na nje.
Akizungumza leo, Novemba 2, 2026, katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati (ADIPEC 2026) unaofanyika Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Dkt. Homera amesema Tanzania imeweka mikakati ya kuvutia wawekezaji katika kipindi ambacho usalama wa nishati umekuwa kipaumbele cha kimataifa kutokana na changamoto za minyororo ya ugavi zinazosababishwa na migogoro ya kijiografia na kisiasa.
Amesema Tanzania ina fursa kubwa za uwekezaji kutokana na kuwa na takribani futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia zinazoweza kuendelezwa kupitia miradi ya LNG na Mini-LNG, pamoja na miradi ya uzalishaji umeme ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere (MW 2,115), mradi wa umeme wa jua Kishapu (MW 150), nishati ya upepo mkoani Singida na jotoardhi katika mikoa ya Mbeya na Songwe.

Aidha, Dkt. Homera amesema nafasi ya kijiografia ya Tanzania inaipa fursa ya kuwa kitovu cha biashara ya nishati kikanda kupitia masoko ya umeme ya Afrika Mashariki na Kusini, huku akisisitiza umuhimu wa sera zinazotabirika, mifumo imara ya kisheria, kupunguza urasimu na kuandaa miradi yenye tafiti za kina ili kuongeza ushindani katika kuvutia mitaji ya kimataifa.
Ameeleza kuwa Serikali, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutekeleza Mkataba wa Kitaifa wa Nishati (National Energy Compact) unaolenga kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi wa takribani dola za Marekani bilioni 4.039, huku vipaumbele vikiwa ni uwekezaji katika nishati jadidifu, uimarishaji wa miundombinu ya usafirishaji umeme na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).

Dkt. Homera amesisitiza kuwa utekelezaji wa mikakati hiyo utaiwezesha Tanzania kubadilisha utajiri wa rasilimali za nishati kuwa miradi halisi yenye tija kiuchumi, kuvutia wawekezaji wa kimataifa na kuimarisha nafasi ya nchi katika soko la nishati duniani


More Stories
SGA yaimarisha utoaji huduma bora kwa wateja
NMT yaimarisha kinga dhidi ya moto kwa watumishi
PREMIER BET yaunga mkono uhifadhi wa Mazingira