November 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yaendelea na jitihada za kurejesha Umeme Mbeya,Songwe

Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea na jitihada za kurejesha huduma ya umeme katika Mikoa ya Mbeya na Songwe, kufuatia kuanguka kwa minara ya njia za kusafirisha umeme katika eneo la Inyala, Mkoani Mbeya.

Tukio hilo lililotokea Novemba 21, 2026, limesababisha kukatika kwa huduma ya umeme katika mikoa hiyo, huku wataalamu wa TANESCO wakiendelea na kazi ya kujenga njia mbadala ya kusafirisha umeme ili kurejesha huduma hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Huduma kwa Wateja ya TANESCO Makao Makuu, wataalamu wa Shirika hilo wamekuwa wakifanya kazi tangu jana kuhakikisha huduma ya umeme inarejea kwa wateja wa mikoa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa lengo la jitihada hizo ni kuhakikisha huduma ya umeme inarejea katika mikoa ya Mbeya na Songwe kabla ya mwisho wa siku ya leo, Novemba 22, 2026.

Aidha, TANESCO imeendelea kuwaomba radhi wateja wake kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo, huku ikiwataka kuendelea kuwa na uvumilivu wakati wataalamu wake wakikamilisha kazi ya kurejesha umeme.

Shirika hilo limeeleza kuwa linaendelea kuchukua hatua kuhakikisha huduma ya umeme inarejea kwa wateja wake katika mikoa hiyo.