November 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Umoti:Huhitaji kumpigia mtu simu kupata mafao ya PSSSF

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

MNUFAIKA wa Fao la Uzazi linalotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),Grace Umoti, amesema amepokea mafao yake ndani ya saa 24 baada ya kuwasilisha madai kupitia mfumo wa PSSSF Portal, bila kuhitaji kumpigia simu mtu yeyote kutoka PSSSF.

Umoti amesema alifanikiwa kuwasilisha ombi lake kwa kuingia kwenye mfumo huo na kujaza taarifa zilizohitajika, ambapo baada ya kukamilisha hatua zote, malipo ya Fao la Uzazi yaliwasilishwa ndani ya muda mfupi.
“Ndani ya saa 24 nililipwa mafao yangu,” alisema Bi. Umoti.

Mnufaika huyo ametoa kauli hiyo Novemba 22, 2026, alipofika katika Banda la PSSSF kwenye Maonesho ya TAREX 2026, yanayofanyika katika Ukumbi wa Superdome, Masaki, jijini Dar es Salaam.

Amesema uzoefu wake umempa imani kuwa huduma za PSSSF kupitia mfumo wa kidijitali ni rahisi na zinaweza kumwezesha mwanachama kuwasilisha madai ya mafao bila kulazimika kufika katika ofisi za Mfuko au kumpigia simu mtumishi wa PSSSF.

Aidha, amewahimiza wanachama wa PSSSF, hususan wanawake wanaostahili Fao la Uzazi, kutumia PSSSF Portal kuwasilisha madai yao kwa kuwa ni njia rahisi na yenye uhakika.
“Nilipowaona mko hapa nikaona nije kutoa shukrani zangu. Kweli mnafanya kazi nzuri sana,” alisema Bi. Umoti