
Na Jouce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa wasambazaji, wauzaji, na watumiaji wa dawa za kulevya, akisisitiza kuwa Tanzania si mahala salama kwa biashara hiyo haramu.
Akizungumza leo Juni 26,2025 jijini Dodoma kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete,, Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kikamilifu kukomesha mtandao wa dawa za kulevya nchini.
“Tanzania siyo mahali salama kwa wauzaji, wasafirishaji, walimaji, na hata watumiaji wa dawa za kulevya. Sasa tumeiva – tunakwenda kukomesha biashara hii haramu,” amesema Waziri Mkuu huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi na wadau waliohudhuria.
Akiwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza juhudi, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ya kimkakati kama vile SGR, vituo vya mabasi, bandari na viwanja vya ndege.
“Dawa hizi zinaangamiza nguvu kazi ya taifa. Zinapoteza uwezo wa kimwili na wa kiakili wa vijana wetu. Hili ni janga la kitaifa,” amesema kwa msisitizo.
Akitolea mfano wa mijadala inayoibuliwa na baadhi ya wachumi wanaodai kuwa biashara hiyo inaleta fedha, Waziri Mkuu amesema Serikali haikubaliani na hoja hizo, kwani gharama ya kiafya na kijamii ni kubwa mno.
“Kama tunataka tupate kizazi cha vijana mazezeta, basi turuhusu biashara hii. Lakini Serikali hii haitakubali, kwa sababu hiyo mijadala haina tija,” amesisitiza.
Waziri Mkuu pia ameeleza kuwa jitihada kubwa zimefanyika chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na kuwapatia vifaa vya usafiri ili waongeze ufanisi kazini.
Amesifu mchango wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha Sheria ya Dawa za Kulevya, hatua ambayo amesema imesaidia kuongeza ushindi katika mashauri ya kesi hizo mahakamani.
“Kwa sasa, kati ya kesi 100 zinazofikishwa mahakamani, Serikali inashinda kesi 76. Hili ni jambo la kujivunia,” amesema.
Pia amesema ushirikiano baina ya Mamlaka ya DCEA ya Tanzania Bara na ile ya ZDCEA ya Zanzibar umeimarika, na umeleta matokeo chanya kwenye mapambano hayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (OWM – Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga amesema Serikali imeimarisha operesheni kwa kufungua ofisi za kanda, huku Dodoma ikiwa miongoni mwa mikoa iliyopata ofisi hiyo.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kwa sasa Tanzania haitambuliki tena kama njia ya kupitishia dawa za kulevya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Tunakotoka siyo tulipo leo. Tumeondoka kwenye doa hilo kwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia,” amesema.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema kuna mafanikio makubwa katika ukamataji wa dawa za kulevya.
“Kuanzia Juni 2024 hadi Mei 2025, tumekamata jumla ya kilo 2,301,414.94 za dawa za kulevya. Hiki ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na kilo 2,050,542.73 zilizokamatwa mwaka uliotangulia,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, zilikamatwa kilo 2.3 , wakati kipindi kama hicho mwaka 2023, zilikamatwa kilo 1.965 ongezeko linaloashiria mafanikio ya juhudi zinazoendelea.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi