Na Mwandishi wetu
WATAALAMU wa masuala ya makumbusho na malikale wa Tanzania na Ujerumani wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili juu urejeshwaji wa mikusanyo iliyochukuliwa na wakoloni nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbassi wakati wa ufunguzi wa warsa ya kujadili namna ya kurejesha mikusanyo hiyo inayofanyika Makumbusho ya Taifa la Tanzania jijini Dar es Salaam, William Mwita amesema kuwa kuna mataifa makubwa ambayo yameonesha nia ya kurejesha mikusanyo hiyo, hivyo kuna haja ya kuweka utaratibu mzuri wa urejeshwaji.
Amesema mikusanyo hiyo ikiwa ni pamoja na mabaki ya binadamu, zana za mawe, mabaki ya mimea na wanyama waliotoweka iliyochukuliwa kabla na baada ya ukoloni inabidi irejeshwe nchini kwa utaratibu maalum kwa lengo la kuendelea kuimarisha uhifadhi wa historia na utamaduni wa Taifa la Tanzania.
Mwita ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, amesema lengo la Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Makumbusho ya Taifa la Tanzania ni kuangalia namna mikusanyo iliyochukuliwa inaweza kurejeshwa ama kunufaisha taifa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watalii na kukuza pato la Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt.Noel Lwoga amesema lengo la warsha hiyo ni kukutanisha wadau wa sekta ya makumbusho na malikale ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mifumo sahihi ya urejeshwaji wa masalia ya mikusanyo mbalimbali na kupeana uzoefu ili kurahisisha utekelezaji wa mpango wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa kurejesha mikusanyo iliyopo nje ya Tanzania.
Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Dkt. Regine Hess amesema Serikali ya Ujerumani inatamani kuona wakazi wa maeneo ambako mabaki ya malikale yalichukuliwa wanakua na mtazamo chanya kuhusu mambo yaliyofanyika wakati wa ukoloni na kusisitiza watu wamapaswa kutazama siku za usoni badala ya kujikita kutazama yaliyopita.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito