Na Irene Clemences, TimesMajira
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Andrea Kigwangalla kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) leo amezindua rasmi filamu inayoitambulisha Tanzania ndani na nje ya nchi katika maeneo mbalimbali ya utalii.
Filamu ambayo inaendana na kauli mbiu ya Tanzania Unforgettable (Tanzania isiyosahaulika) ambayo imejikita kuitambulisha Tanzania duniani kote kupitia huduma bora za kitalii na vivutio vilivyopo hapa nchini.
Dkt.Kigwangala amefanya uzinduzi huo katika makao makuu ya Bodii ya Utalii nchini yaliyopo jijini Dar es Salaam.
Amesema,Tanzania imeendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi licha ya changamoto ya uwepo wa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19), kwani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Magufuli ameiongoza vyema nchi katika mapambano bila kuathiri sekta za kiuchumi ikiwemo utalii hapa nchini.
Wziri huyo amesema kuwa, Tanzania imejipanga kuwahudumia vyema watalii watakaowasili nchini na kuhakikisha kuwa wanaondoka salama ili wakifika katika nchi zao wapeleke habari njema kwamba Tanzania ni salama na watalii ambao walisita kuja waje bila woga kwa ajili ya kujionea vivutio mbalimbali.
Pia Waziri wa Maliasili na Utalii amesema,Serikali imeamua kufungua sekta ya utalii kwa kufuata tahadhari zote zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha watalii kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
Wakati wa uzinduzi huo, Waziri huyo ametoa rai kwa Watanzania kuisambaza filamu hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii ikiwemo Twitter, Telegram, Instargram, Facebook, blogu na mingine mingi ili iweze kuwafikia walengwa kwa lengo la kutangaza Tanzania kiutalii katika soko la utalii la kimataifa zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),Devotha Mdachi amesema kuwa, Tanzania kwa sasa imejikita zaidi kutangaza vivutio vya utalii kupitia mitandao ya kijamii, kwa hiyo kuzinduliwa kwa filamu hiyo fupi kutawasaidia kuteka soko la ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo ameongeza kuwa, kupitia filamu hiyo fupi watalii watapata fursa ya kuona utamaduni na maeneo mbalimbali ya kuvutia na kuweza kuchagua sehemu sahihi ya kwenda kutembelea.
Pia amewataka Watanzania hasa watu maarufu kusambaza filamu hizo za dakika moja, dakika tatu, dakika saba na dakika 10 kwenye kurasa zao ili ziweze kufika mbali zaidi na katika maeneo tofauti tofauti duniani.
Uzinduzi huo ni hatua mahususi na mikakati kabambe ya Bodi ya Utalii nchini kuhakikisha kuwa, Tanzania inapiga hatua kubwa kupitia sekta ya utalii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati