Na Penina Malundo, Dar es Salaam
SERIKALI ya Tanzania na Zambia yapitisha mapendekezo ya kuimarisha ulinzi wa bomba la Mafuta la TAZAMA ikiwemo kuongeza askari katika njia inalopita bomba hilo ,kuhamasisha wanavijiji kuwa walinzi wa kwanza,kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo Drone na Kamera za CCTV.
Pia nchi hizo zimekubaliana kuweka ratiba ya utekelezaji wa mapendekezo hayo yaliyotolewa na Wataalam wa nchi zote mbili, ndani ya siku 45 yawe yametekelezwa.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,Waziri wa Nishati Januari Makamba alisema nchi ya Tanzania na Zambia zinamradi wa muda mrefu ulioanzishwa na Marais Waanzilishi wa nchi zote mbili Keneth Kaunda na Rais Julius Kambarage Nyerere kuanzisha bomba hilo la mafuta.
Makamba amesema miaka ya  nyuma Bomba hilo la mafuta lilikuwa linasafirisha mafuta ghafi yasiyosafishwa na kuelekea nchini  Zambia ambapo huko kuna mtambo wa kuyasafisha mafuta hayo ili yawe mafuta safi na kuwa tayari kwa kutumia katika magari na mitambo mingine .
‘’Miaka ya hivi karibuni,Serikali ya Zambia iliamua kubadilisha bomba hili kuacha kusafirisha mafuta ghafi na kutaka kuanza kusafirisha mafuta ya diseli na kutokana na hali hiyo walianza kufanya manunuzi ya kuwezesha bomba hilo kubadilishwa na imechukua gharama kubwa,’’amesema
Amesema unaposafirisha mafuta ya Diseli ni lazima kuwepo kwa umakini kwani  njiani bomba litakapochokonolewa na  watu kuchepusha mafuta hayo ni hatari kubwa zaidi.‘’sasa tumeamua serikali zetu mbili kufanya utaratibu wa usalama wa bomba,tumetembelewa na Waziri wa Nishati wa Zambia,Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mambo ya ndani wa Zambia  pamoja na wataalamu wao wakiwemo makatibu wakuu wa wizara hizo na wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama wanchi hizo mbili kujadili kwa kina juu ya usalama wa bomba hilo na kutoa mapendekezo yatakayotuongoza,’’alisema.
Amesema hatua ya Zambia kubadilisha matumizi ya bomba hili kutoka kutumika kusafirisha mafuta ghafi hadi kufikia mafuta ya Diseli ni maamuzi makubwa na ya msingi na kufanya Tanzania kuendelea kuwa soko na njia ya kuhakikishia Zambia kuwa na  usalama wa mafuta na bandari kutumika .
Kwa Upande wake Waziri wa Nishati nchini Zambia,Eng Peter Kapala ameishukuru Serikali ya Tanzania katika mkutano huo na kusema kuwa ni muhimu kutekeleza mapendekezo hayo kwa muda waliojiwekea.
Mbali na bomba hilo pia wanatarajia kununua gesi kutoka nchini Tanzania ili kuweza kufanya kufika katika nchi yao na kuweza kutumia katika matumizi mengine.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti