Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI ya Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika Februari 21-22 mwaka huu , katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam ambapo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema , Mkutano huo utahudhuriwa na viongozi kutoka nchi 25 zinazozalisha kahawa Barani Afrika, ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Nchi, Mawaziri wa Kilimo, na wawakilishi wa sekta binafsi na taasisi za kahawa.
Alisema Mkutano huo unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya Kahawa Afrika,” huku mada kuu ikiwa ni mikakati ya kuhamasisha ajira kwa vijana kupitia sekta ya kahawa.
Kwa mujibu wa Bashe,Mkutano huo utatoa mwongozo wa jinsi ya kushirikiana na Umoja wa Afrika na Mashirika yake,
Benki za Maendeleo za Afrika na taasisi nyingine za fedha ili kuunda programu zinazochochea
ujasiriamali na ajira kwa vijana kupitia Sekta ya Kahawa.
Bashe alisema, Serikali ya Tanzania tayari imeanza utekelezaji wa mpango wa ujasiriamali kwa vijana kupitia program ya “Jenga Kesho Iliyo Bora” (BBT), ikiwemo kuanzisha migahawa ya kahawa inayotembea ili kuongeza matumizi ya kahawa nchini,maduka ya kahawa yanayotembea” kwa lengo la kuchochea na kuongeza matumizi ya kahawa nchini.
Alisema ,migahawa hiyo, inawawezesha vijana wajasiriamali kujiajiri kwa kuuza kahawa katika maeneo mbalimbali ikiwemo barabarani kwa wapita njia, kwenye matukio ya umma na kijamii, vyuo Vikuu na hospitali.
” Pia, kuanzisha Vituo vya Umahiri vya Kahawa kwa kushirikiana na taasisi za Elimu ya Juu ili kutoa elimu kwa vijana kuhusu mnyororo mzima wa thamani wa kahawa kutoka uzalishaji hadi kwenye unywaji. “
Vile vile Bashe alisema,Mpango wa kuanzisha Mkutano wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika ni matokeo ya azimio lililopitishwa wakati wa Mkutano wa 61 wa Mwaka wa IACO uliofanyika Kigali, Rwanda, 18 Novemba 2021, la kuandaa mkutano wa ngazi ya juu wa nchi 25 zinazozalisha kahawa Barani Afrika ili kutathmini mapungufu na changamoto zinazosababisha kudumaa kwa wa Sekta ya Kahawa Barani Afrika.
Waziri huyo alisema , Mkutano huo wa Tatuutajadili maeneo muhimu katika mnyororo wa thamani wa kahawa kwa ajili ya kufungua fursa za biashara na ajira kwa vijana.
Aidha alisema usajili wa kushiriki katika Mkutano huo unapatikana mtandaoni kupitia https://www.g25coffeesummit.or.tz huku akisema tarehe ya mwisho ya usajili ni 10 Februari 2025.
Ametumia fursa hiyo kutoa Rai kwa Wadau wa kahawa kujisajili Ili waweze kushiriki katika Mkutano huo ambao utakuwa na manufaa makubwa hapa nchini.
More Stories
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba
Ng’ombe 10 wamekufa kwa kupigwa na radi
Rukwa waanzisha utalii wa nyuki