December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania kuwa kitovu cha biashara mtandao ukanda wa Afrika Mashariki

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

TANZANIA imejipanga kuwa kitovu cha biashara mtandao katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kama ilivyosisitizwa kwenye azimio la Afrika la mwaka 2020 kuhusu kuibadili Afrika kidigitali.

Hayo yamesema jijini hapa leo,Januari 18,2023 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, wakati wa maadhimisho ya siku ya Posta Afrika ambapo amesema Tanzania itafungua vituo vya pamoja vya huduma mbalimbali za Posta.

Maadhimisho hayo yamefanyika Jijini hapa kwa kubeba kauli mbiu “Posta mwezeshaji mahiri wa biashara mtandao inayovuka mitandao barani Afrika.”.

Amesema kuwa Tanzania imejipanga kuwa kitovu ca biashara ya mtandao ambayo imekuwa kipaumbele cha Afrika yote, kama ilivyosisitizwa kwenye azimio la Afrika la mwaka 2020 kuhusu Kuibadili Afrika Kidijitali.  

Ameeleza kuwa Azimio hilo linataka kuwepo kwa Soko Moja ya Kidijitali Afrika ifikapo mwaka 2030, ambapo hapatakuwa na mipaka ya watu, bidhaa, huduma na mitaji Barani humu.

“Tanzania imetunga na kuweka mifumo ya kisera, kisheria na kiusimamizi inayolenga kuendeleza biashara mtandao nchini na kati yake na nchi nyingine Afrika,

“Hiyo ni pamoja na kuendeleza uwekaji na uendeshaji wa miundombinu katika maeneo yote yanayohusiana na biashara mtandao ma hilo hufanyika kupitia utoaji wa leseni na uwekaji wa sera zinazochangia biashara mtandao, kama vile Sera ya Teknolojia Hanari na Mawasiliano (Tehama) ya 2016,

“Pia kutunga Sheria ya Miamala Mtandaoni ya mwaka 2015 ambayo imeboreshwa mwaka 2022 lengo likiwa ni kuimarisha usalama na imani,vitu ambavyo ni muhimu kwenye shughuli za biashara mtandao,”amesema

Vilevile wameadhimisha miaka 43 ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU),amesema Tanzania ina imani kuwa huduma za Posta zitawezesha kuibadili Afrika Kidijitali kama ilivyokusudiwa katika Azimio la Umoja wa Afrika (2020-2030). 

“Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha biashara mtandao katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati; na hatimae kufungua vituo vya pamoja vya huduma mbalimbali za Posta,”amesema

Nape amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya jitihada zinazochukuliwa na sekta ya Habari na Mawasiliano katika kuleta mabadiliko chanya ya kiuchumi hapa nchini.

“Rais Samia ameonesha azma ya ziada katika kuendeleza matumizi ya mfumo wa Taifa wa anwani za makazi na postikodi. Kwa kuanzia, alihakikisha kuwa mfumo huo unatumika ipasavyo wakati wa utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022,

“Rais amekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono ujenzi wa jengo la makao makuu ya PAPU jijini Arusha, ambalo litakapokamilika, na kuanza kutumika, litaongeza ufanisi wa Umoja huo katika kutoa huduma na pia litazalisha ajira zaidi kwa Watanzania,”amesema Nape

Pamoja na hayo amesema kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itahakikisha kuwa huduma za Posta nchini zinazidi kuboreshwa na kukua ili kuendana na mapinduzi ya teknolojia Duniani.

Kwa upande wake Mkurugezi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA)Dkt.Jabir Bakari amesema kuwa Tanzania imepata heshima kubwa kutokana na jengo la makao makuu ya PAPU kujengwa kwenye Ardhi ya Tanzania Jijini Arusha.

Kwani jengo hilo litatoa ajira nyingi na fursa nyingi za kibiashara.

Naye Katibu wa PAPU,Dkt.Sifundo Chief Moyo amesema kuwa maadhimisho ya Miaka 43 ya Umoja wa Posta Afrika huadhimishwa tarehe 18 Januari, kila mwaka huku yakiwa na lengo la kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya Posta kubadilishana salamu na kutakiana heri ya Mwaka Mpya.

“Katika kipindi ambacho Dunia tunayoishi ni ya mapinduzi ya kidigitali ambapo sekta ya Posta nayo imezidi kupanua wigo wa huduma zake,”amesema Chief Moyo.

Huku Kaimu Posta master mkuu,Ferdinand Kabyemelwa akizungumza katika maadhimisho hayo amesema kuwa Posta imedhamiria kujiendesha kibiashara ikiwemo kuvuka mipaka kwani Miundombinu ipo.