May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Burundi akiagana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya mazungumzo yao kwenye Ikulu ya Gitega ambako alihudhuria mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Tanzania kuisaidia Burundi kuwa mwanachama wa SADC

Na Mwandishi Maalumu, Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU, Kasim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kuisaidia nchi ya Burundi ili ifanikiwe katika adhma yake ya kutaka kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama ilivyoombwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza wakati wa uhai wake .

Rais wa Burundi , Evariste Ndayishimiye akizungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwenye Ikulu ya Gitega nchini Burundi baada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Marehemu Pierre Nkurunziza Juni, 26,2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Ijumaa, Juni 26, 2020) alipozungumza kabla ya mazishi ya Rais Nkurunziza yaliyofanyika kwenye uwanja wa Ingoma uliopo Gitega nchini Burundi, Mheshimiwa Majaliwa alisema ameshiriki mazishi hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

“Marehemu Rais Pierre Nkurunziza alitamani sana kukabidhi madaraka huku akiwa ametimiza kiu yake ya kutaka Burundi iwe mwanachama wa SADC jambo ambalo halikuwezekana naamini Mheshimiwa Rais utalisimamia suala hilo hadi  litimie”.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete wakitoa heshima baada ya kuweka mashada ya maua kwenye kaburi la aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza katika mazishi yaliyofanyika Gitega nchini Burundi, Juni 26, 2020. Wa pili kushoto ni Mama Salma Kikwete na wa Nne kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Elibariki Maleko.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Alisema Rais Dkt. Magufuli amemtuma afikishe salamu za pole kwa mke na familia ya marehemu,  Rais wa Burundi  na wananchi wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza kilichotokea Juni 9, 2020.

Waziri Mkuu alisema Tanzania  na Burundi ni ndugu na anaamini undugu na mshikamano huo utaendelea kuwepo hata baada ya kifo cha Rais Nkurunziza ambaye alitoa mchango mkubwa katika kuuimarisha mshikamao  huo.

Alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi kumpa ushirikiano Rais wao mpya Evariste Ndayishimiye  kama walivyofanya  kwa marehemu  Nkurunziza ili aweze kuliongoza Taifa hilo vizuri.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye akimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza kabla ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre, Nkurunziza yaliyofanyika Gitega, Juni 26, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Naye, Rais wa Burundi, Ndayishimiye  alisema Serikali yake itayaenzi na kuyaendeleza mema yote yaliyofanywa na Marehemu Nkurunziza na aliwashukuru viongozi wote kutoka nje ya nchi yake ambao walishiriki katika mazishi hayo.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye (wa tatu kulia ) akiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwenye uwanja wa Ingoma uliopo Gitega kabla ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, Juni 26, 2020. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mama Salma Kikwete, Mjane wa Marehemu Nkurunziza, Denise Nkurunziza na Mke wa Rais wa Burundi Angeline Ndayubaha. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Rais Mstaafu  wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, mkewe Mama Salma Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.

Alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura jana asubuhi Juni 26, 2020, Mheshimiwa Majaliwa alipokelewa na Waziri Mkuu wa Burundi, Prosper Bazombaza.

Baada ya mazishi hayo Mheshimiwa Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Burundi  kabla ya kurejea nyumbani. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete wakizungumza na Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombaza wakati walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bujumbura na baadae walisafiri kwenda Getega kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, Juni 26, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)