June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania Kuadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani Juni 14, 2025

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Serikali kupitia wizara ya afya imedhamiria kuadhimisha Siku ya Wachangia Damu Duniani kwa kufanya kampeni ya kitaifa ya uchangiaji damu, itakayofanyika tarehe 14 Juni 2025 katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kuchangia damu kwa hiari na kuongeza upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha.

Akitoa tamko hilo leo Juni 12, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kampeni ya mwaka huu inalenga kukusanya zaidi ya chupa 41,325 za damu kupitia ushiriki wa wananchi, taasisi, na wadau mbalimbali wa afya.

Aidha Mhe. Mhagama amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya kutambua na kushukuru wachangia damu kwa moyo wao wa huruma na kujitolea kuokoa maisha ya wengine.

Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Tanzania ilikusanya chupa 578,827 za damu, sawa na asilimia 98 ya mahitaji ya taifa, hatua ambayo Waziri ameielezea kama mafanikio makubwa.

“Kwa niaba ya Serikali, nawapongeza na kuwashukuru wachangia damu wote nchini. Mmeokoa maisha ya watoto wachanga, wajawazito, majeruhi wa ajali na wagonjwa waliokuwa katika uhitaji mkubwa wa damu,” amesema Waziri Mhagama.

Amesisitiza kuwa damu haiwezi kutengenezwa viwandani na kwamba ni zawadi ya maisha kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, akihimiza wananchi kutembelea vituo vya damu salama vilivyo karibu kwa ajili ya kuchangia damu.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Changia Damu – Leta Matumaini – Kwa Pamoja Tunaokoa Maisha.”