November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania, India kufungua fursa mpya za biashara

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Tanzania na India zimeonesha dhamira ya kufanya kazi kwa karibu katika kutafuta njia bora za kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amesema kufunguliwa kwa soko la parachichi nchini India mwaka 2022 ni miongoni mwa mifano ya hatua zilizochukuliwa za kuimarisha biashara kati ya Tanzania na India.

Balozi Mbarouk amesema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 74 ya Jamhuri ya India zilizofanyika tarehe 26 Januari 2023 katika Ofisi za Ubalozi wa India Jijini Dar es Salaam.

“India ni mshirika wa tatu kwa ukubwa wa kibiashara na Tanzania na imekuwa miongoni mwa wawekezaji watano bora kwa kuwekeza Dola za Kimarekani bilioni 4.58 kwa mwaka 2021/22. Usawa wa kibiashara katika mwaka huo ulikuwa sawa na miradi 630 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 3.68 iliyozalisha ajira mpya 60,000,” alisema Balozi Mbarouk.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa wawekezaji wa India wameonesha nia ya kuwekezaka nchini Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile madini, utalii, viwanda, kilimo, usindikaji wa mazao ya kilimo, nishati, usafirishaji, ujenzi, huduma za fedha na maendeleo ya rasilimali watu umekuwa ukiongezeka kwa kasi.

“Sekta nyingine wawekezaji wa India walizowekeza nchini Tanzania ni pamoja na afya, elimu, maji, teknolojia ya Habari na mawasiliano. Mfano, Mwezi Juni 2022 tulishuhudia kampuni sita kutoka India zikisaini kandarasi ya uchimbaji wa visima vya maji katika miji 28 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 500, kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha watanzania milioni sita (6) kupata maji safi na salama,” aliongeza Balozi Mbarouk.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na India katika kuendeleza na kuimarisha misingi ya ushirikiano iliyowekwa na waasisi wa Mataifa yetu mawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mahatma Gandhi.

“tutaendelea kutafuta maeneo mapya yenye fursa za kushirikiana ili kuimarisha zaidi ushirikiano wetu wa kijamii, kiuchumi na kisiasa,” aliongeza Balozi Mbarouk.

Kwa upande wake Balozi wa India nchini, Mhe. Binaya Srikanta Pradhan amesema India imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania ambapo uhusiano huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa mataifa yote mawili.

Balozi Pradhan alisema kuwa katika kipindi cha baada ya uhuru, uhusiano kati ya India na Tanzania umestawi na kuchochea misingi ya kuongezeka kwa uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kwa pande zote mbili.

“Tunaendelea kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha nchi hizi mbili zinakua kiuchumi, hivyo ushirikiano wa India na Tanzania ni muhimu katika kukuza uchumi na kuhakikisha maendeleo yanaimarika,” alisema Balozi Pradhan