December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania inatilia mkazo Afya ya uzazi,mama na mtoto kupitia miongozo na mikataba mbalimbali

Na Penina Malundo 

TANZANIA ni miongoni mwa nchiĀ  imesaini mikataba mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda ambayo ina lengo la kuboresha afya ya uzazi, mama na mtoto.

 Lengo namba 3 la Maendeleo Endelevu (SDG 3), kipengele cha 7 linazungumzia upatikanaji wa huduma za afya uzazi kwa wote, ikiwemo uzazi wa mpango, kupata habari zinazohusiana na afya ya uzazi na kuweka afya ya uzazi katika mipango ya serikali, ifikapo mwaka 2030.

Aidha,katika  Kifungu namba 14 (g) cha Itifaki ya Maputo (Maputo Protocol) kinazungumzia haki za afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake.

Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu anasema serikali imekuwa ikitekeleza mikataba hiyo ya kimataifa kwa kuingiza masuala ya afya ya uzazi mama na mtoto katika mipango yake yote kuanzia Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano (2021/2022 ā€“ 2024/2025) na Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya (2021/2022 ā€“ 2024/2025). 

Mipango hii yote inatekelezwa na Wizara kupitia Mpango mmoja wa Taifa wa afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Lishe (One Plan III) ambapo katika  mpango huo kuna Mpango Maalum wa uwekezaji katika afya ya Uzazi kwa Vijana na Kupambabana na Unyanyasaji wa Kijinsia na Unyayasaji dhidi ya Watoto (National Accelerated Action And Investment Agenda For Adolescent Health And Wellbeing – NAIA-AHW) 2021/22 ā€“ 2024/25).

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo inaendelea na safari yake ya  utekelezaji wa mikataba na miongozo mbalimbali ya Kitaifa ikiwemo wa Itifaki ya Maputo ya Afya ya Uzazi wa Kijinsia kwa Wanawake.

Waziri Ummy anasema nchi ya tanzania inatilia mkazo  afya ya Uzazi, mama na Mtoto kupitia miongozo mbalimbali  ikiwemo wa Maputo Protocol.” Wizara inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa tunatekeleza haki za Afya ya Uzazi katika shughuli zetu za kila siku na tunafanya kazi na wadau mbalimbali wakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali kwani wanaelewa kuwa afya ya uzazi sio tu kuwa ni huduma bali pia ni haki ya msingi katika ustawi wa jamii,”anasema.

Anasema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 serikali ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango 2,538,247 sawa na asilimia 89 ya lengo, sindano za uzazi wa mpango aina ya Depo-provera dozi2,564,691 sawa na asilimia 94 ya lengo na vipandikizi 552,494 sawa na asilimia 81 ya lengo. 

Waziri Ummy anasema pia, serikali imeendelea kuwapelekea wananchi huduma hizi kwa kufanya huduma za mkoba (outreach services) ambapo asilimia 18 ya wateja wa njia za uzazi wa mpango walipata huduma kupitia njia hii katika kipindi hicho.

Anasema kuongezeka kwa matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango  kunadhihirishwa na takwimu za mwaka 2021/2022 (DHS / MIS) ambapo matumizi hayo yameongezeka kutoka asilima 32 (TDHS 2015/16) hadi kufikia asilimia 38(DHS/MIS 2022/23).

”Pamoja na kutoa huduma za uzazi wa Mpango, Wizara imeendelea kuandaa miongozo, kanuni, sera na sheria mbalimbali zinazowezesha utoaji wa haki za afya ya uzazi kwa wanawake na vijana nchini,”anasema na kuongeza

“Ili kuboresha huduma za afya ya uzazi, tunahitaji kupata taarifa sahihi na njia salama, zenye ufanisi, nafuu na zinazokubalika katika upangaji waujauzito kwa kuchagua hivyo basi ni lazima wananchi wapewe taarifa sahihi ili waweze kujikinga na mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa,”anasisitiza.

Kwa Upande wake Mkuu wa Ubora na Uboreshaji wa Sekta ya Afya na Umma kutoka Hospitali ya Maria Stopers,Dkt. Selemani Mbyallu kutoka Hospitali ya Maria stopers, anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imeingia mikataba mbalimbali katika kuhakikisha afya ya uzazi wa mpango inasimamia na kuwafikia wananchi mbalimbali.

” Tanzania  hadi inapongia katika makubaliano ya kimataifa uwa inamaanisha  kitu wanachokifanya kama ukiangalia makubaliano ya  Maputo Protocal,ilivyohakikisha inasimamia ipasavyo makubaliano yao mbalimbali waliyojiwekea kama nchi mwanachama  katika vipengele vya kuhakikisha Tanzania inasimama na masuala ya afya ya uzazi wa mpango na kuhakikisha watanzania wanapanga uzazi,”anasema 

Anasema kuna vipengele ambavyo tayari wameanza kuvifanyia kazi katika makubaliano mbalimbali kama uhakikishaji wa utoaji wa huduma ya afya ya uzazi wa mpango bure katika vituo vyao vya serikali na kuhakikisha watoa huduma kupatiwa mafunzo maalum ambayo yataweza kuwasaidia katika utoaji wa elimu kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo,”anasema 

Anasema ni kweli kuna baadhi ya vipengele ambavyo hadi sasa bado hawajaweza kukabiliana navyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ambayo mifumo ya Tanzania bado inashindwa kuchukua hatua madhubutu kutokana na changamoto mbalimbali.

” Tanzania  ni miongoni mwa mwanachama  wa makubaliano mbalimbali ikiwemo Maputo Protocol ambapo kuna vipengele vingi ambavyo vipo na tumeanza kuvitekeleza ipasavyo na pia kunavipengele vingine  ni vingumu kuvicopi na kunavipengele vingine mifumo yetu bado haijaanza kuruhusu na kushindwa kuvichukua,”anasema 

Anasema kuna baadhi ya vitu vinakuwa vigumu kutokana na asili ya nchi,mila na desturi katika maisha yanayowazunguka watu lakini pia ipo vipengele vingine ambavyo bado Tanzania haijawafikia ambapo Tanzania inapambana katika kuhakikisha afya ya uzazi wa mpango.