Na Jovina Bujulu, TimesMajira Online-MAELEZO
NCHI ya Tanzania imetimiza miaka 59, tangu ili ilipojipatia uhuru wake mnamo Desemba 9, mwaka 1961. Uhuru huu ulitokana na jitihada kubwa zilizoongozwa na muasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kishirikiana na viongozi wengine ambao walipigana kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha uhuru unapatikana.
Uhuru wa Tanzania una maana pana kwa Watanzania kwani katika kipindi cha miaka hiyo 59, wameshuhudia maendeleo makubwa ambayo yawagusa katika kiwango cha mtu mmoja mmoja na Taifa zima kwa ujumla.
Katika kitabu chake cha Uhuru na Maendeleo, Mwalimu Nyerere anasema kuwa, ”Uhuru na Maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana, uhusiano wao ni sawa na uhusiano baina ya kuku na yai !, Bila kuku hupati mayai ; bila mayai kuku watakwisha. Vile vile bila uhuru hupati maendeleo, na bila maendeleo ni dhahiri kwamba uhuru wako utapotea”.
Maneno hayo ya Baba wa Taifa ni mfano wa maendeleo ambayo Watanzania wameendelea kuyashuhudia hasa katika kipindi cha Serikali ya Awamu yaTano, chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli ambapo mambo mengi yamefanyika yaliyoliwezesha Taifa la Tanzania kupaa kiuchumi hadi kufikia uchumi wa kati.
Mafanikio ya Tanzania kufikia uchumi wa kati yalitangazwa na Benki ya Dunia kuanzia tarehe 1, Julai, 2020, ambayo ni tarehe ya mwaka mpya wa fedha na hivyo kuifanya Tanzania kujiunga na mataifa saba, ya eneo la Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara. Suala hili limekuja mapema sana ambapo kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo Tanzania, ilipangwa kuingia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Kwa Tanzania kufikia uchumi wa kati kabla ya muda uliyopangwa ni kiashiria cha wazi kuwa maendeleo ya Tanzania yanaakisi maneno ya Baba wa Taifa kuwa uhuru na maendeleo ni vitu vinavyohusiana sana, kwa sababu maendeleo yaliyopatikana nchini kwa haraka yameweza kuinua maendeleo ya nchi, mwananchi mmoja mmoja na uchumi kwa ujumla.
Maendeleo ya nchi huzaa uchumi imara na kukuza uwezo wa nchi kujiamini pamoja na wananchi wake. Mfano dhahiri wa maendeleo ni jinsi nchi yetu ilivyoweza kugharimia Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni ambapo imetumia shilingi bilioni 331.1 ambazo ni fedha zilizopatikana kutokana na vyanzo vya mapato ya ndani.
Kitendo cha Tanzania kugharimia Uchaguzi Mkuu kimeonesha jinsi nchi yetu ilivyopiga hatua kubwa ya maendeleo kwa sababu kimezifanya hata nchi za kibeberu kushindwa kuingilia uchaguzi wetu na kutuamulia mtu wa kumchagua kutokana na kutowaomba fedha zozote kwa ajili ya ufadhili kutoka katika nchi zao au kutoka katika Jumuiya za Kimataifa.
Viashiria mbalimbali vya maendeleo vinaonekana pia katika kuwakwamua wananchi kiuchumi kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania ( TASAF). Mpango huu umeweza kufanikisha lengo namba moja la malengo 17 ya maendeleo endelevu la kutokomeza umaskini.
Kupitia mpango huu Tanzania imeshuhudia wananchi walio wengi wakijikwamua kiuchumi na kuweza kumudu mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na uhakika wa kupata Bima ya Afya, uhakika wa kupata chakula na umiliki wa mali jambo ambalo ni muhimu katika kutokomeza umaskini.
Katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, Tanzania imeendelea kushuhudia maendeleo mbalimbali ambayo yanahusisha watu na Taifa zima kwa ujumla. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema katika nukuu mojawapo kwamba, “ Wananchi wanapaswa kuhusishwa kufikia maendeleo ya kweli, hakuna Taifa lenye haki ya kufanya maamuzi kwa ajili ya Taifa lingine, hakuna watu kwa ajili ya watu wengine, kazi ndio msingi wa maisha na maendeleo yataletwa na kazi”.
Nukuu hii ya Mwalimu Nyerere inasadifu kauli ya Rais Magufuli kuhusu kufanya kazi ili kujiletea maendeleo. Kauli mbiu ya Serikali yake ni ‘ Hapa Kazi Tu’, ambapo tunaona kuwa tangu aingie madarakani mwaka 2015, amewahamasisha watu kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo hivyo kuinua kipato cha familia zao.
Aidha, kutokana na uongozi imara wa Rais Magufuli, wananchi wameweza kuendelea na kuchapa kazi kwa bidii bila kubugudhiwa na mtu yoyote. Mfano hai ni jinsi wafanyabiashara ndogo ndogo, mama lishe na baba lishe wanavyoendesha shughuli zao bila bugudha yoyote. Wafanya biashara hawa wamepewa vitambulisho vya wajasiriamali ambavyo vinawawezesha kufanya biashara katika sehemu yoyote nchini Tanzania ambayo wameruhusiwa.
Kutokana na kukua haraka kwa maendeleo, Tanzania imeshuhudia kuimarika kwa huduma mbalimbali za kijamii kama vile upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mengi nchini, upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo mengi nchini hususan vijijijni ambapo mpaka sasa zaidi ya vijiji 9,000 kati ya vijiji 12,000 vimekwisha patiwa umeme na vijiji vingine vinaendelea kupatiwa umeme.
Huduma nyingine za kijamii zilizoimarika ni pamoja elimu bure kwa kutoka elimu ya msingi mpaka sekondari, huduma za afya, ambapo Seikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani iliongeza bajeti ya Wizara ya Afya kutoka bilioni 30 hadi kufikia bilioni 369, hatua iliyolenga kuboresha afya za wananchi kwa kuwa hakuna maendeleo kama watu watakuwa na maradhi.
Maendeleo mengine yanashuhudiwa katika uboreshaji wa miundombinu ambapo Serikali imeweza kusimamia ujenzi na matengenezo ya barabara katika miji yote ya mikuu ya mikoa kuunganishwa na barabara za lami, vivuko na madaraja.
Serikali ya Awamu ya Tano, pia imejikita katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ni pamoja na mradi wa kuzalisha umeme wa Nyerere katika mto Rufiji, ujenzi wa treni ya kisasa (SGR), kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), mradi wa miundombinu na miradi ya umeme. Madhumuni ya miradi yote hii ni kuwezesha shughuli za maendeleo ya kijuchumi na kijamii.
Katika kusisitiza umuhimu wa maendeleo na uhuru, Mwalimu Nyerere alisema katika mojawapo ya nukuu zake alisema kuwa “ Maendeleo ni yetu na ni juu yetu wenyewe, yataletwa na watu, yaendeleze watu, yawafae watu”. Nukuu hiyo inaonesha jinsi maendeleo yanavyoweza kutafutwa na watu na yakawafaa watu wenyewe.
Hii inawezekana kwa kufanya kazi kwa bidii ambapo nchi itakuwa na uwezo wa kujiamulia mambo yake yenyewe na hivyo kuondokana na dhana ya kuwa ombaomba kwa mataifa ya nje pamoja na wafadhili.
Hivyo wakati Tanzania ikitimiza miaka 59 ya uhuru, Watanzania wanajivunia maendeleo mbalimbali yaliyopatikana na yanayoendelea kupatikana. Aidha Tanzania inashuhudia kuwa kutokana na maendeleo hayo, nchi inaendelea kujiletea heshima duniani na kutembea kifua mbele kwa kudumisha uhuru na umoja.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia