Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Kigoma
RAIS wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Burundi Evarist Ndayishimiye wamekubaliana mambo sita kwa ajili ya kuleta maendeleo katika nchi zao.
Akizungumza baada ya kufanyika kwa mazungumzo hayo ambayo yamefanyika Ikulu ndogo ya Kigoma nchini, Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye amesema mambo hayo ni miundombinu kwa upande wa reli, barabara, usafiri wa majini, biashara, madini, ufugaji pamoja na ulinzi na usalama.
Amesema, wamejadiliana kwa kina kuhusu masuala ya kisiasa , kiuchumi na kiutamaduni na wamekubaliana kuendeleza biashara ya madini na katika kufanikisha hilo wamekubaliana mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote mbili kuitisha mkutano mapema kujadili masuala hayo.
Pia wamekubaliana kuimarisha miundombinu ya barabara, reli pamoja na bandari ambapo katika eneo la reli wataunganisha reli kutoka Uvinza , Msongat hadi Itenga yenye urefu wa kilometa 200.
Katika mazungumzo yao wamebaini katika eneo la kibiashara bado nchi hizo hazijatumia vizuri fursa zilizopo kwa kila nchi, hivyo wamekubaliana kuendelea kudumisha biashara na kwa ngazi ya kikanda wamezungumzia hali ya usalama katika maeneo ya maziwa makuu ambapo wamekubaliana kudumisha umoja.
Wakati kwa upande wa kimataifa amesema, wamekubaliana kukumbushana ajenda ya Afrika kuhusu maendeleo. Kuhusu wakimbizi, amesema hivi sasa wakimbizi wengi wanarudi Burundi kwani hali ya amani na usalama imeimarika.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema, Rais Ndayishimiye amechagua Tanzania kuwa nchi yake ya kwanza mara tu ya kuchaguliwa, ameonesha heshima kubwa lakini inaonesha ni jinsi gani Tanzania na Burundi wamekuwa ndugu.
Amesema, hiyo ni hatua nzuri kama nchi katika kuleta maendeleo na kitendo cha Burundi kupewa fedha dola milioni 23 za ujenzi bandari ya Burundi Bujumbura kunaonesha kuaminika kwa nchi hiyo ambayo uchumi wake umeanza kuimarika.
Rais Magufuli ametoa mwito kwa Warundi waendelee kushirikiana katika kujenga nchi yao kwani ina rutuba nzuri, madini ya kutosha na ina amani.
Amesema, wamezungumzia madini ya Nicol ambayo yapo katika eneo Msangati nchini Burundi na kwa upande wa Tanzania yapo eneo la Kabanga.”Katika eneo hili la madini ya Nicol tutajenga kiwanda cha kuchenjua madini ya Nicol ili kuyaongezea thamani na kisha kuyauza na kupata fedha.
“Leo nimezungumza na Rais Ndayishimiye kuhusu kuruhusu madini ya Burundi kama dhahabu yawe yanakuja kuuzwa hapa Kigoma, kwa bahati nzuri sisi tunayo maduka ya kuuza madini,” amesema Rais Magufuli.
Akizungumzia kuhusu reli, Dkt. Magufuli amesema kupitia watalaam wa reli nchini Tanzania wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Masanja Kadogosa , hawatashindwa kufanikisha ujenzi wa reli hiyo ambayo itatokea Uvinza hadi Itega na reli hiyo itakapokamilika itatumika kusafirisha madini ya Nickel.
“Bidhaa za Burundi zinasafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salam kwa asilimia 98 na itakuwa vema zaidi iwapo bidhaa za nchi hizo zitakazopitishwa bandari ya Dar es Salaam ikafikia asilimia 100 ili wafanyabiashara wasiwe wanapata tabu,”amesema Rais Magufuli.
Aidha amesema kuwa, katika mwaka 2016 biashara kati ya Burundi na Tanzania zilikuwa ni bilioni 115.15 na kwa sasa imefikia bilioni 20.Amesema kituo cha uwekezaji nchini kimesajili miradi 16 kutoka Burundi yenye thamani ya dola za Marekani milioni 29.42 na imetoa ajira kwa zaidi ya watu 544 huku kampuni 10 kutoka Tanzania yamewekeza nchini Burundi.
Wakati huo huo Rais Magufuli amezindua rasmi jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na kushuhudiwa na Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye.Baada kuzindua jengo hilo amesema litarahisisha upatikanaji wa huduma ya haki kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma.
More Stories
Samia, Mwinyi wawapa miezi mitatu wawekezaji
Tanzania,Uingereza kushirikiana katika kuendeleza madini Mkakati
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi