March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tantrade yawaita wawekezaji wa ndani, nje kuwekeza uboreshaji wa uwanja wa maonesho Sabasaba

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetoa wito wa kuwakaribisha wawekezaji wa ndani, kimataifa, taasisi za fedha, wadau wa
sekta binafsi na mashirika ya maendeleo kuchangamkia fursa ya kushiriki kuendeleza Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J.K. Nyerere maarufu kama Viwanja vya Sabasaba, na kuvigeuza kuwa kituo cha kisasa cha biashara na uwekezaji.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tan Trade, Latifa Khamis wakati wa utambulisho rasmi wa mradi wa kuendeleza uwanja wa maonesho wa mwalimu Nyerere.

Amesema TANTRADE imetambulisha rasmi mpango wa kuendeleza uwanja huo
wa maonesho kuwa kituo cha maonesho cha kisasa na chenye hadhi ya kimataifa sambamba na kuufanya kuwa kituo cha maonesho ya biashara cha kisasa( Business
Exhibition and Commercial Hub for Africa).

Amesema uwanja huu utakuwa kivutio si tu cha wafanyabiashara, bali pia cha watalii wa biashara (business tourists), wawekezaji, na wadau mbalimbali wa maendeleo duniani.

Khamis amesema mradi huo unatarajia kugharamu kiasi cha Dola za Kimarekani Milion 322, huku kusudio la kuendelezwa kwa uwanja huo ni kuliweka eneo hilo kuwa kitovu cha biashara na maonesho barani Afrika “A Business Hub”.

Amesema uwanja huo utakapokamilika utachochea uchumi wa taifa kupitia shughuli mbalimbali kuanzia ujenzi, utoaji
huduma, ajira, biashara ndogo na kubwa.

“Mradi huu mkubwa tunatarajia
kuutekeleza kupitia ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).” amesema Khamis na kuongeza kuwasisitiza wadau wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya dhati kujitokeza kufanya uwekezaji

Amesema Tan trade wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Ofisi ya PPP Center (PPPC), wakipata ushauri wa kitaalamu na kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa tija, uwazi na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Khamis amesema TanTrade, kwa kushirikiana na Ofisi ya kukuza ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) ambayo imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji, yenye uwazi, weledi na ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha mradi huu unakuwa wa mafanikio

“Kwa wawekezaji wenye nia ya kushiriki, kigezo cha awali cha kuwasilisha nia ya
uwekezaji ni pamoja na nyaraka ya Nakala zilizothibitishwa za usajili wa kampuni na maelezo ya mawasiliano ya wawakilishi wakuu,Wasifu wa kampuni (Company Profile) itakayoonesha uzoefu katika miradi ya aina inayofanana na huu, muhtasari wa nia ya uwekezaji (Investment Expression of Interest)ukiainisha malengo ya jumla ya uwekezaji,dhana ya maendeleo (development concept), ratiba ya utekelezaji wa mradi,makadirio ya gharama za uwekezaji wa miundombinu (CAPEX),
Kipindi cha mkataba wa kuendeleza mradi (concession time),mapato au manufaa yatakayolipwa kwa TanTrade kupitia
upangishaji wa ardhi na mgao wa mapato.

“Vigezo vingine ni pamoja na Ushahidi wa uwezo wa kifedha wa mwekezaji kwa kuwasilisha ripoti za fedha zilizokaguliwa kwa miaka mitatu mfululizo amesema Khamis na kuongeza mradi huu unatarajiwa kuanza kutekelezwa ndani ya miezi 18 tangu kusainiwa kwa mkataba pamoja na kuwasilisha dhamana ya benki (bank guarantee)

Aidha ametaja maeneo makuu yatakayoendelezwa
kupitia mradi huu ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maonesho ya kisasa: tutajenga miundombinu ya maonesho yenye viwango vya kimataifa ili kuendana na mahitaji ya sasa ya biashara za ndani na za kimataifa

“Miundombinu hii itajumuisha Kumbi za maonesho za ndani zenye viwango vya kimataifa,zikiwa na nafasi kubwa, mifumo ya kisasa ya taa, mawasiliano na huduma za kielektroniki (ICT) kwa ajili ya wafanyabiashara,
taasisi na washiriki kutoka mataifa mbalimbali,maeneo ya wazi ya maonesho yenye mpangilio bora na huduma
muhimu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na mifumo ya kidijitali itakayowezesha uendeshaji wa shughuli za
maonesho kwa ufanisi kuanzia usajili wa washiriki, huduma za malipo, mpaka mifumo ya taarifa kwa wageni na washiriki,”amesema Khamis.

Kwa upande wake Kamishna wa Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP),David Kafulila ameipongeza TanTrade kwa kutumia mfumo wa PPP, na kusema kuwa inatoa fursa kwa Tanzania kuongeza mtaji wa sekta binafsi, teknolojia ya hali ya juu na utaalamu wa usimamizi.

Amesema PPP itashirikiana na TanTrade katika kuvutia na kufanya biashara na sekta binafsi kupitia mfumo wa PPP.
“Mradi huu umekuja wakati muafaka wakati Tanzania ikijitahidi kuwa na uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo 2050,”

Amesema ili kufikia lengo hilo, nchi inahitaji sekta za viwanda, viwanda na huduma zenye ushindani wa kimataifa. Maonesho ya kimataifa ya biashara yatakuwa muhimu katika kuendesha mauzo ya nje, kuvutia uwekezaji, na kukuza ushirikiano wa kikanda.

Ameongeza mradi huu ni mkubwa na uamuzi wa Tantrade kutaka sekta binafsi kufanya hivi ni changamoto kutoka sekta za serikali kwamba sio kila kitu wanachotaka kufanya waombe Hazina .