Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE)imesema katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kuziwezesha Kampuni 234 za Tanzania kujitangaza katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa ya biashara nchini Msumbiji, Komoro, Oman, China, Indonesia na mataifa mengine.
Ambapo ushiriki huo umeimarisha upatikanaji wa masoko mapya kwa bidhaa za Tanzania, mikataba ya kibiashara na uwekezaji wa kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo Machi 13,2025,Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE ,Latifa Mohamed Khamis,kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita amesema kuwa mafanikio hayo kwenye masoko ni bidhaa za Tanzania kama kahawa, chai, bidhaa za urembo, nguo, na mavazi zilipata soko jipya nchini Msumbiji.
Amesema katika masoko hayo Itifaki ya kibiashara ilisainiwa, kurahisisha upatikanaji wa fursa kwa bidhaa za nyuki (asali) katika soko la China.
Aidha Latifa amesema TANTRADE imefanikiwa kufanya mafunzo ya wazalishaji wa zabibu yaliyounganisha wafanyabiashara wa zabibu 200 na viwanda 13 vya kusindika zabibu jijini Dodoma ambapo iliwezesha kupata soko la jumla ya tani 2,500 za zabibu zilizokuwa zimekosa soko kufuatia ongezeko la mavuno.
Ametaja wakulima walionufaika kuwa ni wa Vijiji Mpunguzi, Mkulabi, Matumbulu, Hombolo, Chibelele, Makang’wa, Mvumi na Veyula.
Vilevile amesmea kuwa Mamlaka hiyo inaratibu ushiriki wa nchi kwenye Maonesho ya Expo 2025 Osaka yatakayofanyika kuanzia tarehe 13 Aprili, mpaka 13 Oktoba, 2025 Osaka, Japan.
“Ushiriki wa Tanzania umejikita katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini kwenye Sekta za kipaumbele ikiwemo Afya, Nishati, Madini, Utalii, Kilimo, Uchumi wa Buluu, Sanaa na Utamaduni pamoja na juhudi za Serikali za kuwezesha Uwekezaji na biashara ikiwemo miradi ya kimkakati ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege na nishati ya umeme na gesi.
Akizungumzia mwelekeao wa Mamlaka hiyo Latifa amesema kuwa wanampango wa kujenga uwezo wa Taasisi kujiendesha kwa ufanisi ambapo imekamilisha mpango mkuu wa uwekezaji katika uwanja wa maonesho wa mwl. J. K. Nyerere ambao unatarajiwa kuboreshwa kuwa wa kisasa kuendana viwango vya kimataiafa.
“Uwekezaji katika uwanja huu unatarajia kuwa na utaratibu wa Ushiriki wa Sekta binafsi na sekta ya Umma yaani Public, Private Partnership – PPP ili kufanikisha hilo,Mamlaka imejipanga kusajili mradi huo na kutafuta wabia katika uwekezaji wake kutoka nchini na nchi za nje. Kwa kuzingatia hilo, Expo 2025 Osaka Japan ni sehemu muhimu ya kupata wabia hao ili kufanikisha uwepo wa majengo ya kisasa ya maonesho,”amesema Latifa.




More Stories
Vyombo vya ulinzi na usalama Mbeya,Benki kuu kushirikiana kutatua changamoto za utapeli mtandaoni
Polisi Mbeya kuimarisha ulinzi kuelekea sikukuu ya Pasaka
BAKWATA yawazawadia washindi wakuhifadhi Qur’an