Na Penina Malundo,Timesmajira,online
WIZARA ya Viwanda, Biashara na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) zimezindua nembo ya Taifa ya viungo kwa lengo la kuongeza tija katika bidhaa hiyo.
Akizungumza katika maonesho hayo mwishoni mwa wiki Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe kwenye maonesho ya 45 ya Biashara amesema asilimia 60 ya Watanzania wamejiajiri katika shughuli za kilimo, hivyo katika mpango wa serikali wa kutaka sekta binafsi iwe muwekezaji mkuu wa uchumi wa viwanda nchini ni vyema bidhaa ya viungo navyo vikapewa kipaumbele.
Akizungumzia kuhusu namna serikali inavyosaidia sekta hiyo, amesema wameanza kuondoa vikwazo na tozo mbalimbali ambazo si za lazima ili kuondoa urasimu.
Katika kuondoa hilo amesema, wameanzisha mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo mitandao ambao unasaidia kupunguza ukiritimba uliokuwepo kwenye baadhi ya taasisi za serikali.
“Tunakwenda kwenye uchumi wa ushindani kama Rais, Samia Suluhu Hassan katika mpango wa maendeleo wa tatu wa miaka mitano, ambao tunataka tuwe na uchumi shindani wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu na maendeleo hayo hayatofanikiwa iwapo kama hatutakuwa na bidhaa zenye viwango ikiwemo viungo,” amesema.
Amesema serikali kwa sasa inalenga kufanyabiashara na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zilizo Kusini mwa Afrika na baadaye soko huru la biashara Afrika.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha bidhaa za viungo vya chakula ambazo zitakwenda kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi, kuna aina zaidi ya 30 ya viungo zinazozalishwa nchini na kuanzia sasa Tanzania imejikita kuboresha aina tano ambazo ni karafuu, mdalasini, pilipili manga, hiliki na tangawizi hii ni kwa upekee kwa sababu mazao haya yamekuwa yakifanya vizuri katika soko la ndani na nje ya nchi,” amesema.
Akizungumzia kuhusu nembo ya Taifa ya viungo, amesema itasaidia kutambulisha mazao kitaifa na kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Balozi Mteule Edwin Rutageruka amewashauri wadau wa kahawa kutumia mfumo wa uuzaji wa bidhaa kwa mitandao ulioasisiwa kati ya Shirika la Posta na TanTrade.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19