January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANROADS Tabora wakarabati barabara zote zilizoathiriwa na El-Nino

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKAZI wa Wilaya za Kaliua, Urambo, Sikonge na Uyui Mkoani Tabora wamempongeza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani hapa kwa kurejesha mawasiliano ya barabara zote zilizoathiriwa na mvua za el-nino.

Wametoa pongezi hizo wiki hii kwa nyakati tofauti mbele ya waandishi wa habari waliokuwa katika ziara maalumu ya kuangalia hali ya miundombinu ya barabara katika wilaya zote za Mkoa huo.

Justin Msanze mkulima, mkazi wa Kijiji cha Kangeme, Kata ya Ukumbisiganga Wilayani Kaliua, amesema kuwa barabara ya Kaliua-Lumbe ni miongoni mwa barabara muhimu sana katika wilaya hiyo ambayo ilikatika na kusababisha adha kubwa kwa wananchi.

Amebainisha kuwa barabara hiyo ambayo inaunganisha Mkoa wa Tabora na Katavi kupitia wilaya hiyo ni kiungo muhimu sana kwa usafiri na usafirishaji mazao ya wakulima na bidhaa za wafanyabiashara hivyo walipata adha kubwa.

‘Tunamshukuru sana mama yetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia TANROADS fedha za kutosha ili kurejesha mawasiliano ya barabara hii, kwa sasa inapitika vizuri baada ya kufanyiwa matengenezo’, ameeleza.

Amos Mtemo, mwendesha bodaboda mkazi wa Kijiji cha Ugansa, Kata ya Usinge Wilayani Kaliua amemshukuru Rais Samia kwa kuipatia TANROADS fedha za kutengeneza barabara inayounganisha Kijiji hicho na kata kwa kiwango cha lami.

‘Barabara hii yenye urefu wa km 7.4 ni muhimu sana kwetu, lakini wakati wa masika ilikuwa kero kubwa, tunashukuru kwa kuwa wanatuwekea lami, mkandarasi yuko hapa anaendelea na kazi, asante sana mama yetu,’ amesema.

Mohamed Luzige mkazi wa Kijiji cha Ndorobo Wilayani Urambo ameeleza furaha yake kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo ikiwemo kujengwa barabara ya mzunguko ili kuwaondolea adha wananchi.

Mama Sada Mustapha mkazi wa Kata ya Shitage Wilayani Uyui na Lucia Lukala mkazi wa Ipole Wilayani Sikonge wamempongeza Meneja waTANROADS kwa kuchukua hatua za haraka kumaliza kero iliyokuwepo ya kukatika barabara zao.

Akiongea kwa niaba ya Meneja wa TANROADS Mkoani hapa, Mhandisi Christephola Nichombe amekiri barabara nyingi kuathiriwa na mvua hizo ila akabainisha kuwa wamefanya kila juhudi kurejesha mawasiliano ya barabara hizo.

Ametaja baadhi ya barabara zilizoathirika sana na kusababisha mawasiliano kukatika kuwa ni ya Kaliua-Lumbe, Ipole-Rungwa, Sikonge-Mibono-Kipili na Mambali-Bukumbi-Shitage-Mhulidede.

Amebainisha kuwa barabara hizo sasa zinapitika, baadhi zimekamilika na nyingine wakandarasi wanaendelea na matengenezo ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi za wananchi zinaendelea kama kawaida.

Amesisitiza kuwa Mheshimiwa Rais anajali sana wananchi wake hivyo TANROADS Tabora haitamwangusha, itaendelea kuhakikishia barabara yoyote inayokatika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha inafanyiwa matengenezo ya dharura ili kutokwamisha shughuli za maendeleo.