May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makampumi yanayouza mbolea feki kitanzini

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKULIMA wa zao la tumbaku Wilayani Kaliua Mkoani Tabora wamemwomba Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuyafutia usajili makampuni yanayosambaza mbolea iliyochakachuliwa kwa wakulima.

Wametoa ombi hilo jana walipokuwa wakiongea na Waandishi wa habari waliotembelea vijiji vya Usindi na Usimba katika kata za Ushokola na Usimba Wilayani humo ili kujionea maendeleo ya kilimo cha zao hilo kabla ya masoko.

Baadhi yao wamekiri kupata mafanikio makubwa katika kipindi cha msimu uliopita wa 2022/2023 kutokana na juhudi kubwa za serikali ya awamu ya 6 zilizowezesha mbolea kupatikana kwa wakati na wanunuzi kununua kwa bei nzuri.

Joseph Ntahondi mkulima, mkazi wa Kijiji cha Usimba na Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Usimba amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa kusimamia vizuri sekta ya kilimo, sasa manufaa yanaonekana.

Amebainisha kuwa msimu uliopita walivuna kilo laki 9 za zao hilo na kuuza kati ya dola za kimarekani 2.4 hadi 3 kwa kilo na matarajio yao kwa mwaka huu ilikuwa kuvuna kilo milioni 1au zaidi lakini wana wasiwasi kama watafikia kiwango hicho.

Ameafanua kuwa msimu huu baadhi ya wakulima tumbaku yao haikustawi vizuri, mbolea waliyotumia haikuwa na ubora hivyo kudumaza zao hilo, tofauti na iliyotumiwa na wenzao katika maeneo mengine.

‘Baadhi ya makampuni yanatuletea mbolea iliyochakachuliwa, ambayo ni feki, hawa hawatutakii mema, tunaomba Waziri Bashe awachukulie hatua stahiki na ikiwezekana wafutiwe usajili au leseni ya kuuza mbolea za pembejeo’, ameeleza.

Peter Daniel mkulima, mkazi wa Kata ya Usimba amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 kupitia Waziri mwenye dhamana za kuinua wakulima, ila akasikitishwa na baadhi ya makampuni kufanya mchezo mchafu wa kuwauzia mbolea feki.

‘Mwaka jana tulipata mbolea za pembejeo kwa wakati na kwa bei nzuri na tukapata kilo za kutosha, ila haya makampuni yanataka kuturudisha nyuma kimaendeleo, tunamwomba Waziri au Mama yetu awapige marufuku kuuza mbolea’, amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Usindi, Haji Masudi amekiri kuwa zao la tumbaku limeleta neema kubwa kwa wananchi kwani kila aliyelima mwaka jana amejenga nyumba nzuri na wengine wamenunua pikipiki na magari.

Ameshukuru serikali kwa kukomesha vitendo vya ubadhirifu vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya viongozi wa Amcos na kuongeza kuwa kila mkulima sasa anapata stahiki zake kulingana na kilo alizozalisha ila akasikitishwa na baadhi ya makampuni yanayochakachua mbolea.

Meneja wa Chama Cha Msingi Usindi, Mohamed Abdallah amesema kuwa serikali imetoa mwongozo wa usimamizi thabiti wa vyama vya msingi hivyo hakuna Kiongozi yeyote anayeweza kudhulumu mkulima, akithubutu cha moto atakiona.

Mwakilishi wa Meneja Mkuu wa Chama Cha Ushirika Milambo, Lucas Kalonga amempongeza Rais Samia kwa kutafuta makampuni mengi ya kununua zao hilo, thamani ya tumbaku sasa imerudi, inauzwa kati ya sh 4800 hadi 6000 kwa kilo.

Amebainisha kuwa uzalishaji wa zao hilo katika Wilaya za Urambo na Kaliua umeongezeka mara dufu kwani mwaka juzi jumla ya kilo mil 17 zilizalishwa, mwaka jana kilo mil 32 na mwaka huu wanatarajia kuvuna zaidi ya kilo mil 60.

Amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na serikali katika kusimamia zao hilo ili wakulima waendelee kunufaika zaidi, aliomba Waziri mwenye dhamana ya kilimo kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuuza mbolea feki.