Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,Tanga
SERIKALI kupitia Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima imeonesha kuridhika kwake na dhamira ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) chini ya kampuni tanzu ya Sisalana Tanzania Limited kwa kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wakulima wa mkonge.
NSSF kupitia kampuni ya Sisalana ambayo ilianzishwa maalumu kwa ajili ya kusimamia shughuli zote zilizokuwa zinafanywa na kampuni ya Katani katika usindikaji wa mkonge, ilichukua baadhi ya mali za kampuni hiyo ambazo ziliwekwa kama dhamana ya mkopo uliotolewa na NSSF kwa nia ya kurejesha fedha za wanachama.
Akizungumza na waandishi wa habari Wilayani Korogwe mkoani Tanga, Malima alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeweka mkakati mahususi wa kuzalisha zao la mkonge kitaifa kutoka tani 35,000 hadi tani 120,000.
“Mkakati huu unasimamiwa na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) lengo lake kupitia uzalishaji wa mkonge, mkulima awe anashiriki kama mmiliki wa uzalishaji kupitia AMCOS (Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao),” alisema.
Alisema Serikali imeanza kwa kuijengea uwezo AMCOS ili iweze kuzalishaji kwa wingi na kwamba ina mmbia katika uzalishaji huo ambaye ni kampuni ya Sisalana iliyo chini ya NSSF.
Alisema kampuni ya Sisalana lazima ijijenge uwezo wa kupokea mkonge unaotoka kwa mkulima ambapo sasa inapokea tani 6,000 za mkonge kwenye AMCOS zote, lakini ina uwezo wa kupokea tani 11,000 na hivyo kwa kushirikiana na timu yake wametengeneza mkakati ili hizo tani 11,000 za katani ziweze kuifikia kampuni ya Sisalana kwa ajili ya kuchakatwa na mkulima apate haki yake.
Malima alisema lengo la ziara hiyo ni kueleweshana kuhusu umuhimu wa zao hilo kwani Mkoa wa Tanga unazalisha tani 20,000 za mkonge, hivyo ipo haja ya kuongeza uzalishaji na kufikia tani 60,000, kwani katani inayotoka Tanzania ndio namba moja kwa ubora duniani.
“Nawaomba wakulima waendelee kulima kwa wingi kwani NSSF kupitia kampuni ya Sisalana itaichakata katani yote kwa ubora unaotakiwa,” alisema.
Malima alimuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kuhakikisha uongozi wa AMCOS unaendana na unasimamia malengo ya wanachama ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Alisema Serikali inawahamasisha wakulima waendele kulima na kuzalisha katani kwani kampuni ya Sisalana ipo kwa ajili ya kuichakata na Bodi ina wajibu wa kuhakikisha masoko yanapatikana.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Balozi Ali Iddi Siwa, alisema Sheria iliyoanzisha NSSF inawaruhusu kuingia katika uwekezaji, ambapo kampuni ya Sisalana imepewa majukumu ya kuendesha korona tano kwa madhumuni ya kurudisha fedha ambazo NSSF ilikopesha kampuni ya zamani ya Katani Limited.
“Kwa hiyo Sisalana imeingia ili iweze kurejesha fedha hizo za wanachama na inaendesha shughuli za biashara kwa kushirikiana na AMCOS ambapo kazi yetu kubwa ni kuchakata majani ya katani ili AMCOS ziweze kuuza ‘brash’ ambayo inaitwa singa na sisi (NSSF) tunapata tozo kutokana na kuchakata,” alisema.
Alisema lengo lao ni kutanuka zaidi katika biashara ya mkonge na tayari Sisalana wana mikakati ya kuendelea mbele ambayo NSSF inaiunga mkono ili mradi iwe inafuata taratibu na kanuni za uwekezaji ambazo zinatawala Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi