Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SHIRIKA la Umeme Tanzania(TANESCO)limesema limeanza ujenzi wa kujenga laini kubwa ya kilovoti 400 ambayo itabeba umeme kutoka Chalinze mpaka Zuzu-Dodoma.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 26,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwakani 2026 na ndiyo itakuwa mwarobaini wa changamoto nyingi za umeme ambazo zipo sasa.
“Kwasasa tunao mradi ambao tumeanza kujenga kwajili ya kuwa na laini kubwa ambayo itabeba umeme kutoka Chalinze ili iweze kuleta mpaka Dodoma na ukifika Dodoma uingie kwenye Substion ya Zuzu ambayo ndiyo Substion mama katika mfumo wetu wa Gridi ya taifa,”amesema Mha.Gissima.
Mha.Gissima amesema kuwa umeme huo ukishakuwepo kutakuwa na uhakika kwamba huo umeme unaotoka Julius Nyerere unaweza sasa wote kubebwa na ukafika Dodoma na ukasambazwa kwenda kwenye maeneo yote ya nchi kwa kadri ya mahitaji ya matumizi.
Amesema kuwa mradi huo umefadhiliwa na serikali ya Tanzania na umeanza kutekelezwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita na hadi sasa umefikia asilimia 15.
Vilevile Mha.Gissima amesema kuwa wanamradi wa kuunganisha gridi ya taifa na gridi ya mataifa jirani ili kuwa na kapu la pamoja la umeme.
“Gridi yetu na Kenya imeungana maana yake ni kwamba mfumo wetu wa umeme utaungana na nchi nyingi ambazo zipo katika ukanda wa Kaskazini Mashariki mwa Bara la Afrika.Kwa maana ya Kenya yenyewe kwenda Ethiopia, Sudani ya Kusini kwenda Uganda na kadhalika,”amesema.
Aidha amesema kuwa wanamradi mwingine ambao utaunganisha na mfumo wa Tanzania na mfumo wa gridi wa nchi za Kusini mwa Afrika ambazo zinitwa nchi za SADC.
“Na tunachotaka kufanya pale kuwa na kapu la pamoja ambapo mradi huu umeanza kuanzia Iringa,miundombinu mikubwa ya umeme ya kilovoti 400 inajengwa kutoka Iringa mpaka Mbeya,Mbeya hadi Tunduma halafu Tunduma inavuka kwenda Zambia ukishafika Zambia tunajiunganisha na Gridi ya nchi za SADC.
“Mradi huu umeshaanza Km 624 zitajengwa lakini pia utekelezaji wake umefikia asilimia 34 ba mradi huu unapofika pale Tunduma maana yake tutairefusha ile laini ya msongo wa kilovoti 400 ili iweze kwenda Sumbawanga na baada ya hapo Mkoa wa Rukwa nao uweze kuingia kwenye mfumo wa gridi ya taifa na tunatarajia hili litakamilika mwaka 2026 hadi 2027,”amesema Mha.Gissima.



More Stories
Rais Samia atoa msaada kwa kituo kinachohifadhi wasichana waliokimbia ukatili
Mo Dewji na Urithi anaoujenga ,unavyoenda mbali zaidi ya mafanikio binafsi
Mulika Community kusaidia Serikali kukomesha vitendo vya ukatili