March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanesco yatumia wiki ya huduma kwa wateja kurejesha fadhila kwa jamii

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online -Sumbawanga

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limeendelea kurejesha faraja kwa wananchi kupitia huduma zake za kijamii, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka huu 2025.

Katika Mkoa wa Rukwa, shirika hilo limeunganishia umeme familia ya Safari Ally, wa kijiji cha Pito, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ambaye ana mahitaji maalumu kutokana na changamoto ya kuzungumza.

Mbali na hilo,TANESCO imemkabidhi jiko la umeme linalotumia nishati kidogo, ikiwa ni hatua ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya hiyo ,Salome Safari amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo ambao umewapunguzia ukali wa maisha kwani wana uwezo wa kutumia umeme kujiingizia kipato.

“Ninawashukuru TANESCO kwa msaada huu nitabuni biashara mbalimbali zitakazo niingizia kipato na nitaondokana na changamoto ya kuombaomba,”amesema Salome.

Akizungumza wakati wa tukio hilo,Oktoba 7, 2025,Ofisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Rukwa,Angeline Bidya, amesema kuwa ni utamaduni wa shirika hilo kila mwaka, wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, kurudisha fadhila kwa jamii kwa kutekeleza miradi midogo yenye kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Bidya,amesema TANESCO itaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake na kushirikiana nao katika kulinda miundombinu ya umeme kwa maendeleo endelevu ya taifa.