Na Penina Malundo,Timesmajira
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange amewahakikishia watanzania kuendelea kuwapatia elimu juu ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia.
Katika kutoa elimu hiyo Tanesco leo imetoa zawadi ya majiko ya umeme kwa Wananchi waliofika katika banda lao lililopo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 7,2025 katika viwanja vya maonesho hayo, Mkurugenzi Twange amesema wananchi waliofika katika banda lao wamepata fursa ya kupata elimu ya nishati safi ya kupikia na kupatiwa majiko.

“Ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba watanzania tuhame kwenye kutumia nishati isiyokuwa safi na kutumia iliyosafi, hivyo hapa tunazungumzia nishati ya umeme na tuna majiko haya ya umeme yamefanyiwa utafiti na kuthibitika kuwa unaweza kupikia na chakula kikaiva kwa kutumia chini ya Unit moja tu.
“Kupitia maonesho haya tumeona ni vema wananchi tuwapatie maswali na wale wanaojibu vema maswali waliyoulizwa wamepata fursa ya kujishindia zawadi ya majiko hayo ya kupikia”amesisitiza

Aidha amewashukuru watanzania waliofika katika banda lao na kuwapatia elimu kuhusu masuala ya nishati safi yakupikia.
Naye Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Sadock Mugendi amesema wamekuwa wakisambaza na kusafirisha umeme maeneo mbalimbali vijijini na kwamba hivi karibuni wamemaliza mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tabora mjini kuelekea Katavi wenye kilomita 383 na una msongo wa Kilovolt 132.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako