July 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO kuzalisha megawati 5000 ifikapo 2025 kuuza umeme nje ya nchi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SHIRIKA la Umeme Tanzania(TANESCO)limesema linatekeleza miradi kadhaa ya kuzalisha umeme ambayo itasaidia kuongeza kiwango cha umeme katika Gridi ya Taifa kila mwaka kukiwa na lengo la kuzalisha Megawati 5000 hadi 6000 ifikapo 2025 na kuuza nje ya nchi.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Februari 22,2023 na Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wateja kutoka TANESCO,Martin Mwambene wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu na utekelezaji wa Taasisi hiyo.

Mwambene amesema kuwa uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini ni Megawati 1,820, ambapo kwa sasa mitambo iliyopo inauwezo wa  kuzalisha Megawati 1,300.

“TANESCO inafanya miradi kadhaa ambayo inasaidia kuongeza kiwango cha umeme katika Gridi ya Taifa kila mwaka ambapo malengo ni kufikia Megawati 5,000 hadi 6000 ifikapo mwaka 2025,

“Kwasasa Mradi wa Umeme wa bwawa la Julius Nyerere upo asilimia 88 ambapo sasa hivi tumeanza kujaza maji ambayo yamefikia mita za ujazo 133 kutoka usawa wa bahari,

“Najua Wateja wamekua wakijiuliza TANESCO hawafikirii kutafuta njia mbadala lakini sisi kama TANESCO tumefikiria kuwa na mbinu za miradi mbadala ambayo itaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme ikiwemo ya gesi na jua, pia kuna vyanzo binafsi vyenye uwezo wa kuzalisha umeme mfano viwanda vya sukari,”amesema Mwambene.

Aidha amesema kuwa Miradi ya uzalishaji umeme inaenda sambamba na miradi ya kusafirisha umeme, katika mradi wa JNHPP ambapo kuna njia ya kusafirisha umeme itakayoanzia Rufiji mpaka Chalinze na tayari transfoma kubwa takriban sita zimepelekwa zinasubiri kufungwa.

“Kuna baadhi ya mikoa ikiwemo Rukwa na Katavi haipo katika Gridi ya Taifa, hivyo kuna laini ambazo zitajengwa ambazo zitakuwa zinaunganisha nchi na nchi nyingine karibu nchi nzima itakuwa ipo katika mfumo wa Gridi ya Taifa,”amefafanua.

Mwambene ameeleza kuwa utatekelezwa mradi wa Gridi Imara utajumuisha ununuzi wa mashine umba 6,000, mita laki 7 za umeme, nguzo 380,000, ununuzi na ufungaji wa nyaya zenye urefu wa KM 40,000, ujenzi wa vituo 14 vya kupoza umeme na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme mkubwa takriban KM 948.

“Mradi huu wa Gridi Imara ni ushahidi kwamba matatizo ya umeme yaliyopo nchini tunayafahamu na tunatarajia mradi huu utayatatua,”amesema.

Pamoja na hayo Mwambene amefafanua swali lililoulizwa na Mwandishi wa habari kuwa kumekuwepo na changamoto kwa wateja wapya wanaotaka kuwekewa umeme kutoa gharama za nguzo hadi tatu huku wengine wakipata urahisi wakuunganisha umeme bila gharama za nguzo kupitia nguzo zilizonunuliwa na wateja wengine,

Ambapo Mwambene  alijibu kuwa  TANESCO haiuzi nguzo bali inauza huduma ya umeme hivyo kama mteja atatakiwa kuunganishiwa huduma ya umeme kwakulipia nguzo basi atakuwa amelipia huduma ya umeme.