December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO kuvuna Bilioni 6/- GGML kwa mwezi

Na Mutta Robert,TimesMajira Online,Geita

Shirika la Umeme nchini (Tanesco) linatarajia kuuza umeme katika Mgodi wa kuchimba Dhahabu wa Geita (GGML) wenye thamani ya Shilingi Bilioni Sita kila mwezi baada ya kukamilika mradi wa kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa Kilovoti 220 kutoka kituo kikubwa cha Bulyanhulu na kuufikisha kituo cha kupozea umeme cha Mpomvu mjini Geita.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dkt. Tito Mwinuka amesema mradi huo kutoka Bulyanhulu kwenda Geita ukikamilika shirika hilo litauza umeme Megawati 24 kwenye mgodi wa GGML ambao ni umeme mkubwa kwa mteja huyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dkt.Tito Mwinuka akipokea maelezo ya mradi wa kituo cha Bulyanhulu kwenda Geita kutoka kwa Meneja Miradi wa shirika hilo, Mhandisi Emmanuel Manirabona. (Picha na Robert Mutta).

Amesema kuwa, kiwango hicho cha umeme  kitakachotumika mgodini hapo ni sawa na umeme wote unaotumika katika mkoa mzima wa Morogoro.

Dkt.Mwinuka ameongeza kuwa, Mkoa wa Geita utakuwa ni moja ya mikoa michache muhimu ambao utakuwa unaingizia Tanesco mapato makubwa kila mwezi kutokana na mauzo ya umeme kila mwezi.

Amewataja wateja wakubwa wa shirika hilo  ambao wanatarajiwa kununua umeme zaidi ya Megawati 30 kuwa ni Geita Gold Mining Limited na StamiGold ambayo inatarajiwa kununua Megawati 5.

Meneja wa Miradi wa Tanesco, Mhandisi Emmanuel Manirambona amesema, ujenzi wa mradi wa Bulyanhulu ulipaswa kukamilika mwezi huu kulingana na mkataba,lakini umechelewa kidogo baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 kwa sababu baadhi ya vifaa vya mradi vinaagizwa nje ya nchi na meli zilikuwa haziingii nchini.

Amesema, kwa sasa meli zimeanza kuja nchini, hivyo mradi huo utakamilika kwa wakati kwa sababu mkandarasi wa kujenga njia ya kusambaza umeme ameshakamilisha na sasa yuko katika  hatua ya kusambaza umeme kwa kaya 1,500 walioko kando kando na mradi huo.

Mhandisi,Emmanuel Manirambona amesema, mradi huo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95 na kwa muda mfupi ujao mradi huo utakuwa umekalika na kuweza kuwasha umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Dkt.Mwinuka pamoja na kamati yake ya uongozi ya shirika hilo walikuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya shirika hilo katika Mkoa wa Geita ambayo amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo.