Na Penina Malundo,Timesmajira
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO),imetangaza kampeni yake maalumu kwenye maeneo yote nchini ya kuhamasisha ulipaji wa madeni kutoka kwa wateja wa malipo ya baada na ukaguzi wa mita za Luku kwa wateja wa malipo kabla.
Imesema kuwa kampeni hiyo inaenda sambamba na kufungua dirisha la msamaha wa riba kwa muda wa miezi sita kwa wadaiwa hao ili kuwapa nafasi kulipa madeni yao kwa urahisi zaidi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam,Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Irene Gowelle wakati akiongea na waandishi wa habari alisema kampeni hiyo inaenda sambamba na kuhamasisha ulinzi wa miundombinu ya umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha na kuimarisha uendelevu wa upatikanaji huduma bora ya umeme kwa wananchi.
”Kampeni inaanza rasmi Juni 19,2025 ambayo imepewa jina la “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie”, ikienda sambamba na kaulimbiu isemayo, “Huduma endelevu huanza na wewe”,”amesema.
Amesema malengo ya Kampeni hiyo ni pamoja na kuwahamasisha wateja wa malipo ya baada kulipa madeni yao kwa hiyari kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa na kutoa motisha kwa ulipaji wa wakati ikiwemo msamaha wa riba kwa wateja watakaolipa madeni yao kikamilifu.

”Zoezi hili pia litahusisha ukaguzi wa mita za LUKU kwa lengola kuhakikisha zinafanya kazi vizuri na hazijachezewa na wateja wasio waaminifu.
”Vilevile,kuhamasisha umuhimu wa ulinzi shirikishi wa miundombinu ya umeme kwa kuwajumuisha wananchina kuwapa elimu ya kulinda miundombinu ya Shirika,”amesema.
Amesema Miundombinu hiyo ndio inayowezesha upatikanaji endelevu wa huduma ya umeme kwa ufanisi hasa kwa kuzingatia kuwa ulinzi wa Miundombinu ya Umma ni wajibu wa kila mwananchi.
”Natoa rai kwa wateja wake wote nchini ambao wanadaiwa kutoa ushirikiano kwa kulipa madeni yao kwa wakati na hivyo kutoathiri upatikanaji wa huduma ya umeme kwenye shughuli zao.
”Pia inatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi wa miundombinu ya umeme au uharibifu kwa kushirikiana na vyombo vya dola ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa ukosefu wa huduma ya umeme pamoja na kuzuia hasara kwa Shirika,”amesema.
Gowelle amesema lengo la kampeni hiyo ni pamoja na kuhamasisha ulipaji wa madeni ambapo wana wateja wa aina mbili ambao ni wateja wanaolipa kwanza na wale wanaotumia umeme na kulipa baada.
”Kwa sasa tunayo changamoto ya uwepo wa madeni ya wateja wa malipo ya baada kwa maana ya wateja wakubwa na wateja wa kati ambayo tumeona ni vyema tukitumia fursa hii kuweza kuwakumbusha wateja wetu wote nchi nzima kulipa umeme kwenye bili zao kwa hiari kwa sababu kumekuwa na malimbikizo ya madeni .
“Hivyo kama Shirika madeni haya yanatupa changamoto kuendesha shughuli zetu kwa hiyo tukaona ni wakati mzuri wa kuweza kuwakumbusha wateja wa malipo ya baada kuweza kulipa bili zao za ankara za umeme,”amesema Gowelle .

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako