Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limetoa wito kwa wafanyabiashara hapa nchini, kutengeneza package nafuu kwa wazawa ili kutembelea hifadhi za Taifa kujionea mambo mbalimbali yaliomo ndani ya hifadhi hizo.
Akitoa wito huo Mei 10,2024 Visiwani Zanzibar,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANAPA, PCO Catherine Mbena amesema zipo changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania kutembelea hifadhi zao za Taifa, ikiwemo usafiri.
“Zipo changamoto nyingi kwa Watanzania namna ya kufika maeneo ya hifadhi za Taifa, mfano mzuri Kutoka Zanzibar hadi Serengeti ni parefu na gharama ni kubwa.
“Unapanda boti kutoka Zanzibar mpaka Dar es Salaam, baada ya hapo unapanda basi mpaka Arusha, lakini pia, kuna usafiri wa kwenda Serengeti na ili ufaidi huna budi kupanda magari ya utalii kwa sababu yana raha yake,” amesema PCO Catherine.
Amesema kwa kuona hilo ili kuwawezesha Watanzania kufika maeneo yenye vivutio wakafurahia na wao kama wageni ni vyema wakapunguziwa gharama waweze kufika kirahisi kwenye hifadhi za Taifa.
“Mi ningetoa wito kwa Wafanyabiashara wa Tanzania, hizi gahara za usafiri na mambo mengine, tunatamani ziwe himilivu kwa watanzania ili na wao waweze kujikuta wapo kwenye makundi kama wageni kutoka nje.
“Naomba muichukue hii kama fursa ya kuifanyia kazi, mtengeneze package ambazo Watanzania wanaziweza, najua mwisho wa siku ni biashara na watu wanataka kutengeneza faida, bado naona kuna nafasi ya wafanyabiashara wa Tanzania kutengeneza package za watanzania kutembelea katika hifadhi hizo.
PCO Catherine amesema, kwa kufanya hivyo Kwanza Watanzania watachangia pato la Taifa, lakini pili yale maeneo ya uhifadhi yana raha yake hivyo watafurahia maeneo ya hifadhi zao.
Akizungumzia kuhusu jukumu walilopewa TANAPA, Catherine amesema jukumu kubwa walilopewa ni kuhifadhi maliasili zilizopo katika eneo la hifadhi za Taifa.
Amesema, wakati wanapewa jukumu hilo kulikuwa na hifadhi moja tu ya Serengeti lakini kadri siku zilivyozidi kwenda hifadhi zikaongezeka.
Hata hivyo amesema, eneo likionekana lina maliasili ya kipekee au lina umuhimu wa kipekee na linahitaji kutunzwa kwa ajili ya faida ya watanzania wote lakini faida ya dunia nzima, walikuwa wanaongezewa kwa namna ya uhifadhi unaofanyika katika hifadhi hizo.
Aidha, amesema mpaka sasa hifadhi zimeongeza na kufika 21, kwa hiyo Shirika la Uhifadhi la Taifa ‘TANAPA’ linasimamia idadi ya hifadhi 21.
“Muktadha wa hifadhi za taifa kama tunavyozungumza, ni kila kitu kilichopo ndani ya hifadhi, tunazungumzia wanyamapori, wadudu, utulivu wa maeneo haya pamoja na amali zote zilizopo ndani ya hifadhi za taifa.
“Wakati naanza kazi TANAPA, nilikuwa nashangaa kwamba ukifika kwenye hifadhi ya Taifa huruhusiwi kutoa kigogo ambacho kimechoka kwa sababu si mnyama wala sio mmea ambao unaokua, lakini nikajifunza kwamba ile uwepo wa lile gogo pale ni makazi ya wadudu tayari, ukiliondoa utakuwa umeharibu utaratibu wa wadudu na maisha yao.
“Kwa hiyo tunasema tunatunza kila kitu kilichopo ndani ya hifadhi ya Taifa kwa maana ya kukamilisha ile Ekolojia ya eneo husika,” amesema Catherine.
Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA), lipo Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuuelimisha Umma kuhusu shughuli zinazofanywa na shirika hilo pamoja na kuhamasisha kampeni ya ‘VOTE NOW’ ambayo inahusisha upigaji wa kura kwa hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Kilimanjaro.
Hifadhi ya Serengeti na Kilimanjaro, zinawania tuzo za World Travel Award 2024.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua