January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA kuboresha miundombinu Hifadhi ya Taifa Ibanda- Kyerwa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), linajenga lango la kuingilia watalii (Complex gate) eneo la Kifurusa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ibanda- Kyerwa iliyopo mkoani Kagera.

Ujenzi huo unajengwa na Kampuni ya MJT Crew Co. Ltd JV Sumry’s Enterprises Ltd za hapa nchini, ambao utagharimu fedha za kitanzania Bilioni 3.9 kuhakikisha miundombinu ya hifadhi hiyo inaimarika.

Afisa Uhifadhi Mkuu na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena (katikati), akipata maelekezo na Mhandisi wa mradi ujenzi wa lango la kuingilia watalii (Complex gate), linalojengwa na TANAPA katika eneo la Kifurusa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ibanda- Kyerwa iliyopo mkoani Kagera, Bilal Said (kushoto).

Ujenzi wa lango hilo la Hifadhi utahusisha sehemu ya ukaguzi wa nyaraka na malipo, ofisi za wahasibu, ofisi za askari upande wa kuingia na kutokea, ofisi ya Afisa Utalii na msaidizi wake, ofisi ya Tehama, ujenzi wa barabara kilometa mbili na mifumo ya umeme.

Vilevile, vyoo upande wa kuingia, na kutokea vyenye mashimo 7 ya kawaida 1 walemavu kwa kila jengo, uchimbaji wa visima viwili, fensi ya umeme mita 400, Nyumba 2 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 2), Nyumba 3 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 4), vimbweta 08, sehemu ya kupaki magari makubwa na madogo upande wa kutoka na kuingia lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5400, mfumo wa umeme jua, pamoja na eneo la kupumzikia wageni.

Afisa Uhifadhi Mkuu na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena (wa kwanza kulia), akiwa na baadhi ya timu ya Shirika hilo wakikagua mradi wa ujenzi wa lango la kuingilia watalii (Complex gate), linalojengwa na TANAPA katika eneo la Kifurusa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ibanda- Kyerwa iliyopo mkoani Kagera. Wa kwanza kushoto Mhandisi wa mradi huo Bilal Said akimpa maelezo.

Hata hivyo mradi huo umetoa ajira kwa Watanzania hususani wakazi waliopo karibu na Hifadhi hiyo ili waone manufaa ya uhifadhi katika maeneo yao.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya mradi mara baada ya kukutana na timu ya TANAPA, Mhandisi wa mradi huo Bilal Said amesema mpaka sasa mradi umefikia asilimia 55% na unatarajiwa kumalizika Agosti mwaka huu.

Bilal amesema, changamoto wanayoipata katika kutekeleza mradi huo ni umbali wa sehemu wanapo chukulia mahitaji ya ujenzi.

Naye, Afisa Uhifadhi Mkuu na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena amefurahishwa na hatua zilizofikiwa na mradi huo hadi sasa na kuwataka wakandarasi hao kumaliza mradi huo kwa muda uliopangwa

Inaelezwa kuwa mradi huo ukikamilika utasaidia miundombinu ya kupokelea wageni na ukusanyaji wa mapato kufanyika kwa urahisi hatimaye Hifadhi kuingiza pato la Taifa.