November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tamasha la miaka 93 Haile Selassie kufanyika Novemba 2,2023

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Jamii ya imani ya Rastafari Novemba 2,2023 inatarajia kufanya tamasha la kutimiza miaka 93 ya Mfalme Haile Selassie wa kwanza tangu kutawazwa na kuwekwa wakfu wa kuwa mfalme wao wa Afrika.

Mfalme huyo alitawazwa na kuwekwa wakfu Novemba 2,1930 hivyo katika kusherekea miaka hiyo Rastafari wameamua kufanya tamasha hilo kitaifa mkoani Mwanza katika Kijiji cha Kasamwa Igombe wilayani Ilemela ambapo watapata fursa ya kuwasilisha mafanikio, changamoto,elimu kwa jamii pamoja na wadau mbalimbali juu ya imani yao.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa Mratibu wa matukio maalum Rastafari Mkoa wa Mwanza John Kimori, ameeleza kuwa watakuwa na wageni kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kanda ya Kusini huku wenyeji ikiwa Kanda ya Ziwa pia kutakuwa na wageni mbalimbali akiwemo mgeni wa heshima Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula pamoja na Chifu wa Mkoa wa Mwanza.

John ameeleza kuwa pia watapata fursa ya kueleza kero za jamii kwani kazi ya Rastafari ni kutetea jamii,kuikosoa serikali kwa nia njema.

“Kutakuwa na vitu mbalimbali ikiwemo mambo ya jadi ya asili ya Mwafrika,elimu za Rastafari,ibada maalumu itafanyika kwa ujumla ni maisha halisi na mifumo ya Rastafarian pamoja na kuzindua mfumo rasmi wa kimaendeleo wa wanawake Rastafarian Tanzania nzima ili waweze kujiwezesha kiuchumi na tutazindua umoja wetu rasmi,”amesema.