January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tamasha la kihistoria Ujiji kuchochea utalii Kigoma

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Kigoma

WAKAZI wa Mkoa wa Kigoma wameaswa kutangaza vivutio vya utalii mkoani humo,ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Gombe,inayojivunia wanyama aina ya sokwe na maporomoko ya maji yenye mandhari ya kuvutia.

Alhaji Sheikh Hasani Kabeke,amesema leo wakati wa kuhitimisha tamasha la kihistoria na utamaduni wa Mji Mkongwe wa Ujiji Kigoma,lililolenga kuutangaza mji huo na vivutio vingi vya utalii mkoani Kigoma.

Amesema Mkoa huo umeingia katika historia mpya ya kuandaa tamasha la kwanza la kihistoria na utamaduni wa Mji Mkongwe wa Ujiji,kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii,ili kukuza utalii na kuleta maendeleo mkoani humo.

“Tamasha hili ni mwanzo mzuri wa kuhamasisha maendeleo ya kiutalii na kuchochea uchumi wa Mkoa wa Kigoma.Ni matarajio yetu serikali itatuunga mkono na mkurugenzi uwepo wako hapa umetudhihirishia uungwana wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pia,tunawapongeza Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kwa ushirikiano wao,”amesema Sheikh Kabeke.

Amesema tamasha hilo ni heshima kwa wananchi wa Kigoma na halifungamani na chama chochote cha siasa,linahusisha watu wa vyama vyote na kuonya,siasa ikiingizwa halitapiga hatua na kuwataka wanasiasa kupingana kwa kujenga hoja na kunadi sera zao katika majukwaa yao.

Sheikh Kabeke ambaye alikuwa Mwenyekiti wa tamasha hilo,amesema ni jukumu la kila mwanakigoma,kutangaza na kudumisha vivutio vya utalii vya Ujiji na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla.

“Mji wa Ujiji una zaidi ya miaka 300,kuna majengo ya ibada na misikiti yenye zaidi ya karne tano,kuna kanisa lenye miaka 100 na visima vilivyochimbwa wakati wa utawala wa Waingereza,” amesema Sheikh Kabeke.

Amempongeza Rais Dk.Samia kwa juhudi zake za kushiriki kutangaza vivutio vya utalii,kupitia filamu ya Royal Tour ambayo inalenga kukuza utalii nchini, na katika kuunga mkono juhudi hizo,Kigoma wameamua kuutangaza Mji wa kale wa Ujiji,uliojaa mambo ya kihistoria na utamaduni,hata kabla ya ujio wa Dk.Livingstone mwaka 1871.

Ameeleza Mji wa Ujiji ni nyumbani kwa makabila ya Wakusu,Waluba,Wagoma,Wanya,Karamba,Waha,Wabwari,Wabembe,Waororo, Wahombo,Watongwe na Wamasanze,wasiogope kujinasibu kwa kabila zao na kuwaasa kujenga utamaduni wa kurudi nyumbani kila mwaka kukutana na wazazi,ndugu na jamaa.

Kiongozi huyo wa kiroho ameipongeza Serikali kwa kuufungua Mkoa wa Kigoma,kupitia ujenzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kigoma,mradi wa umwagiliaji Bonde la Lwiche,barabara za Kibondo na Uvinza za kiwango cha lami,zitarahisisha usafiri na kuchochea maendeleo.

Sheikh Kabeke amesisitiza kudumisha amani,utulivu na umoja,wananchi kuendelea kuwa wamoja bila kujali dini,kama ilivyo kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini,wanaishi kwa umoja na kushirikiana.

Katika kilele cha tamasha hilo,tuzo mbalimbali zilitolewa kwa baadhi ya watu waliowahi kutoa michango katika Mkoa na Taifa,akiwemo Sheikh Amri Abeid Kaluta, Mwafrika wa kwanza kuwa Waziri wa Sheria na Waziri wa Utamaduni.

Sheikh Kaluta,alifariki mwaka 1964 akiwa na umri wa miaka 40,ametimiza miaka 100 tangu kuzaliwa huku tamasha hilo likifanikiwa kwa jamii kuonesha umoja na mshikamano katika kutangaza utalii na utamaduni wa Kigoma.