January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU,yasaidia kurejesha hekali 8

Na Ashura Jumapili TimesMajira online Kagera,

Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Rushwa(TAKUKURU),Mkoa wa Kagera imesaidia kurejeshwa kwa hekali 8 za ardhi ya Kijiji cha Bugango Kata Kakunyu Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera,Ezekia Sinkala,amesema eneo hilo lilikuwa limemilikishwa kwa mtu kinyume na makubaliano.

Sinkala,amesema kupitia mkutano wa hadhara uliofanywa na TAKUKURU katika Kijiji cha Bugango kwa lengo la kupokea kero mbalimbali zinazohusiana na rushwa na zenye viashiria vya rushwa Julai 12 mwaka huu, ilipokea taarifa ya kuwa mkazi mmoja wa kijiji hicho anamiliki eneo lenye ukubwa wa zaidi ya eneo alilopewa na kijiji kwa mujibu wa taratibu.

Amesema kwa mujibu wa nyaraka za Kijiji inaonyesha kuwa mwananchi huyo amemilikishwa na Kijiji eneo lenye ukubwa wa ekari 25 huku eneo hilo likiwa na zaidi ya hekari alizomilikishwa.

Pia amesema baada ya kupokea taarifa hiyo ilifanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na idara ya ardhi ulifanyika uhakiki wa eneo hilo kwa kupima upya eneo hilo.

Amesema upimaji huo ulibainika kuwa eneo hilo lina ukubwa wa hekali 33 ikiwa limezidi hekali 8,ambazo zinamilikiwa kinyume na makubaliano ya kumilikishwa hekali 25 tu.

Hata hivyo amesema, baada ya matokeo ya upimaji huo Julai 27 mwaka huu,kupitia maamuzi ya mkutano mkuu wa Kijiji eneo hilo lilirudishwa rasmi kwenye umiliki wa Kijiji Bugango.

Wakati huohuo Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Ezekia Sinkala ,amesema kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu wamefuatilia miradi ya maendeleo 18 )yenye thamani ya bilioni 144.9.

Sinkala,amesema miradi iliyofuatiliwa ni ujenzi wa miundombinu ya maji, ujenzi wa wodi za hospitali, ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari na ujenzi wa mabweni ya sekondari.

Aidha,amesema ufuatiliaji huo unalenga kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa enaendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Vilevila amesema wamebaini miradi 10 kati ya 18 yenye thamani ya bilioni 3.1,kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho sawa na asilimia 55.55 ya miradi iliyofuatiliwa.

Amewasisitiza wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuongeza juhudi katika usimamizi wa miradi husika pia kufanya marekebisho ya mapungufu katika miradi iliyobainika kuwa na mapungufu kwa wakati kama walivyoewa ushauri.