Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imetoa onyo kwa wale wote watakaobainika kufuja mali za umma au kutumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na serikali ya awamu ya 6.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Mhandisi Abnery Mganga alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana ambapo alibainisha kuwa wamejipanga kufanya ufuatiliaji wa kina wa miradi yote.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2024 wamejipanga kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kudhibiti vitendo vya rushwa kwa kufanya ufuatiliaji wa kina wa gharama za miradi yote ikiwemo manunuzi yaliyofanywa.
Ameongeza kuwa mbali na kufuatilia utekelezaji miradi ya maendeleo katika halmashauri zote 8 za Mkoa huo ili kujiridhisha kama thamani ya fedha imezingatiwa pia watafuatilia mapato ya serikali katika maeneo.
‘Tutachukua hatua stahiki kwa wale wote watakaobainika kufuja mali za umma na kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka tutahakikisha wahusika wote wa vitendo vya rushwa wanafikishwa mahakamni’, amesema.
Mganga ameeleza kuwa wataongeza jitihada ya kuzuia vitendo vya rushwa kwa kuhamasisha ushiriki wa wananchi kupitia program yao ya elimishaji umma, kufanya chambuzi za mifumo ya utoaji huduma na kushirikisha wadau kujadili matokeo ya chambuzi hizo ili kuweka mikakati ya kudhibiti mianya ya ufujaji.
Aidha amebainisha kuwa kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki wataendelea kushirikisha makundi mbalimbali ya wananchi kutambua kero zao zenye mianya ya rushwa, kuzichambua na kuzipatia ufumbuzi haraka katika maeneo yao.
Amesema kuwa programu hiyo tayari imefanyika katika kata 6 za Mkoa huo ambapo jumla ya kero 47 ziliibuliwa na kati ya hizo 38 zilipatiwa ufumbuzi na 9 ambazo hazikupatiwa ufumbuzi ziliwasilishwa kwa watoa huduma ili zitatuliwe.
Ametaja sekta zilizolalamikiwa idadi ya malalamiko kuwa ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa 29, Mahakama 2, Polisi 4, Ardhi 4 Afya 4, Maji 2 Elimu 6, Vyama vya Ushirika 4, Ujenzi 3, Misitu 1na Idara nyingine 5.
Kuhusu uchunguzi amesema walipokea malalamiko 62 kati ya hayo 46 yalihusu rushwa ambapo 45 yameanza kuchunguzwa na 18 ambayo hayahusuiani na rushwa umetolewa ushauri wa namna bora ya kuyatatua.
Aidha amesema kuwa kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu wamefungua kesi mpya 2 na kufanya kesi zote kufikia 45 na kesi 5 tayari zimeamuliwa na mahakama.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi