November 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU yaokoa Mil. 39 Kagera

Na Ashura Jumapili, Timesmajira Online, Mwanza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU )Mko wa Kagera wamezuia upotevu wa fedha kiasi zaidi ya milioni 39 katika mradi wa ujenzi wa kituo cha maegesho ya magari makubwa ya mizigo Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kagera Pilly Mwakasege wakati akitoa taarifa ya utekelezaji kuanzia kipindi April hadi Juni mwaka 2023 wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake leo Agosti 10 mwaka huu.

Mwakasege,amesema wasingefanya ufuatiliaji katika mradi huo uliopo Ibura Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani humo kiasi hicho cha fedha kingepotea.

Amesema kutokana na uchunguzi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na Takukuru wameweza kuokoa kiasi hicho cha fedha ambacho mkandarasi alilipwa malipo zaidi kuliko kazi alizofanya ambapo alikuwa kiasi cha zaidi ya milioni 36.5 kwa kazi za kushindilia kifusi cha G15 na G45.

Huku akilipwa kiasi cha zaidi ya milioni 2.7 kama thamani ya nondo zilizokuwa hazijatumika katika ujenzi wa kibanda Cha mlinzi pamoja na vyoo.

Machi 13 mwaka huu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila ,wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya Mkoa huo alifika katika mradi huo ambapo alibaini mapungufu mbalimbali zikiweno taa zilizofungwa katika kituo hicho pamoja na nguzo zilizotumika kwenye uzio.

“Naagiza Takukuru ifanye kazi ya kukagua mradi huu wa kituo cha maegesho ya magari makubwa ya mizigo ili kuweza kubaini mkataba unasemaje kuhusu taa zilizowekwa pamoja na mambo mengine ili kuweza kuona kama mkandarasi ametuibia aweze kuwajibishwa vizuri nahitaji taarifa hiyo ofisini kwangu,”alisema Chalamila.

Takukuru wamefanikiwa kubaini kilichotiliwa mashaka na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Chalamila ,kabla ya kuhamishiwa mkoani Dar -es Salam.