Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga inamshikilia Joseph Jonas Tasia baada ya kumkuta na doti 600 za vitenge nyenye nembo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na vya kawaida vikiwa vimehifadhiwa nyumbani kwake.
Takukuru ilimkamata Tasia Juni 29 saa 3:00 usiku katika mtaa wa Mwasele B kwa kile walichodai kuwa jambo hilo linaashiria kuwa vilikuwa vinaandaliwa katika kufanya ushawishi kwa wapiga kura kuelekea uchaguzi Mkuu wa viongozi.
Baada ya kufanya uchunguzi, Takukuru ilibaini kuwa, Tasia ambaye ni mfanyabiashara wa usatiri wa magari madogo taksi hana duka na wala hafanyi biashara ya kuuza vitenge.
Katika mahojiano na Maafisa wa Takukuru, baada ya mtuhumiwa kukamatwa na mzigo huo, ameshindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kuhusiana na mzigo husika na hata nyaraka za manunuzi ya mzigo huo alizowasilisha hazijitoshelezi na kuongeza mashaka juu ya uhalali wa hivyo.
Kwa sasa uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo bado unaendelea ili kubaini iwapo vitenge hivyo vilikuwa ni kwa ajili ya kuhusika na vitendo vya rushwa katika uchaguzi au ni kwa ajili ya kufanya biashara katika msimu huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa viongozi.
Hata hivyo kwa mujibu wa majirani wa mtuhumiwa huyo bwana ni mwanachama wa CHADEMA ndiyo maana walitoa taarifa walipoona sare za CCM zinateremshwa kwake.
Pia zipo taarifa zisizo rasmi kwamba mzigo huo ni wa mmoja wa watia nia wanaotaka kugombea ubunge na Kamanda mkuu wa Takukuru, Mussa amesema wanachunguza kuhusu madai hayo kuona kama yana ukweli japo mtuhumiwa mpaka sasa kagoma kumtaja mtu aliyemtumia mzigo huo.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote