Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora imetembelea na kukagua jumla ya miradi 11 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya zaidi ya bilioni 28 na kubaini dosari katika utekelezaji baadhi ya miradi hiyo.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tabora,Abnery Mganga,amesema kuwa taasisi hiyo imebaini dosari katika miradi 8 kati ya 11 iliyochunguzwa.
Ameeleza kuwa miradi hiyo,iliotekelezwa katika Wilaya zote za Mkoa huo ni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,katika shule za msingi na sekondari kupitia mradi wa SEQUIP na BOOST.
“Nijukumu la taasisi kuhakikisha fedha zinazoletwa na Serikali zinatumika vizuri na si vinginevyo.Tumebaini dosari nyingi katika miradi hii,ikiwemo kutumika vifaa visivyo na ubora,tumeagiza kusitishwa mara moja kwa kazi iliyokuwa ikifanyika na kuelekeza wahusika wakafanye uthibitisho wa vifaa hivyo,”amebainisha.
Ametaja dosari nyingine kuwa ni mafundi waliopewa kazi hiyo kutokuwa na uwezo, kukosekana elimu ya mfumo wa NEST, unaochangia mafundi (local fundi) kushindwa kuomba kazi hiyo kwenye mfumo na baadhi ya shule kujengwa katika maeneo yasiyo na huduma za kijamii.
Mganga amebainisha hatua zilizochukuliwa kuwa ni kuelekeza Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA),kuandaa semina maalumu kwa ajili ya mafundi (local fundi) na wazabuni ili waelimishwe namna ya kutumia mfumo huo.
Ametaja maelekezo mengine kuwa ni kusitishwa mikataba ya mafundi wote walioshindwa kutekeleza kazi zao ndani ya wakati na kutafutwa wengine wenye uwezo wa kutekeleza kazi hizo.
Aidha amezitaka Halmashauri ambazo miradi yao imetekelezwa katika maeneo yasiyo na huduma za kijamii,kuongeza fedha za kupeleka huduma hizo ili kutoathiri gharama zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji miradi hiyo na waandaaji wa BOQST na kuandaa bajeti inayoaksi uhalisia wa mahitaji ya eneo husika.
More Stories
Ilemela yakusanya bilioni 7, mapato ya ndani
Madiwani Ilemela wapitisha rasimu ya bajeti bilioni 84.3
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele