Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imebaini mianya ya rushwa katika mifumo ya uvunaji na usafirishaji mazao ya misitu na kutaka hatua stahiki zichukuliwe ili kukomesha vitendo hivyo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoani hapa Mussa Chaulo alipokuwa akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake ambapo amesema mianya hiyo imebainika kutokana na uchunguzi uliofanywa na Maofisa wa taasisi hiyo.
Amesema mianya hiyo inachochewa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za uvunaji na usafirishaji mazao hayo hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mapato ya serikali kutokana na usimamizi usioridhisha.
Aidha ameongeza kuwa wamebaini ufujaji wa fedha zinazokusanywa kwenye mazao hayo na kutaka hatua stahiki kuchukuliwa katika mfumo huo ili kukomesha vitendo hivyo.
Katika kukabiliana na vitendo hivyo ametaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kuwa ni kuandaa kikao cha wadau na kupitisha maazimio ya kurekebisha kasoro zote zilizobainika katika mfumo huo.
Kamanda Chaulo amebainisha mkakati mwingine ulioandaliwa na kuanza kutekelezwa na taasisi hiyo kuwa ni kuzuia vitendo vya rushwa katika uvunaji na usafirishaji mazao yote ya misitu.
Aidha amesema katika kipindi cha mwezi Januari-Machi 2023 taasisi imechunguza jumla ya mifumo 11, kufanya warsha 4 na kufuatilia utekelezaji wa miradi 18 yenye thamani ya sh mil 662.7 ambapo miradi 2 ya mil 569.5 ilikutwa na mapungufu na hatua mbalimbali kuchukuliwa.
Katika kutekeleza programu ya TAKUKURU Rafiki amesema wamefanikiwa kutembelea kata 14 na kupokea jumla ya kero 176 ambapo kero 46 zilitatuliwa zikiwemo kusambazwa nguzo za umeme na kujengwa mazizi ya mifugo.
Aidha walipokea malalamiko 97 kutoka taasisi mbalimbali na kuyafanyia kazi ambapo 65 yalihusu rushwa na 32 hayakuwa ya rushwa, taasisi hizo ni Tamisemi 59, mahakama 8, polisi 4, ardhi 6, ujenzi 3, manunuzi 2, afya 3, mazingira 1, taasisi za fedha 3 na nyinginezo 8.
Chaulo alisisitiza kuwa wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kushirikiana na wadau wote katika mapambano dhidi ya rushwa, aliomba jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili kukomesha vitendo hivyo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa