May 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Tabora  wabaini dosari utekelezaji wa miradi 

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  mkoani Tabora, imechunguza miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya bilioni 45 na kubaini dosari katika utekelezaji wa  miradi yenye thamani ya bilioni 17.8.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa wa Tabora, Azza Mtaita,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji majukumu ya taasisi hiyo  kwa kipindi cha miezi 3 (Januari-Machi) kwa  waandishi wa  habari mkoani humo.

Amesema, jumla ya miradi 14 yenye thamani ya bilioni 45.9 ilichunguzwa na kati ya hiyo  miradi 4 yenye thamani ya  bilioni 17.8,ilibainika kuwa na mapungufu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na ubora unaotakiwa na kuchelewa kukamilika.

Mtaita ametaja miradi iliyochunguzwa kuwa ni soko kuu la kisasa linalojengwa katika kata ya Chemchem na stendi kuu ya mabasi inayojengwa eneo la Inala, miradi hii inatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya bilioni 19.

Amedokeza kuwa miradi hii inatakiwa kukamilika ndani ya miezi 12, lakini hadi kufikia Machi 2025 ilikuwa imetekelezwa kwa asilimia 3 tu badala ya 25, hivyo akashauri waongeze kasi na kuzingatia ratiba ya mpango kazi na mkataba wao.

Pia mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora wenye thamani ya bilioni 24.6,ulibainika kuwa na  nyufa kwenye baadhi ya kuta za jengo la abiria hivyo wakashauri kuzibwa nyufa zote, hili limetekelezwa. 

Mtaita amebainisha miradi mingine iliyochunguzwa kuwa ni ya ujenzi wa barabara za lami zilizoko katikati ya Mji wa Tabora,mitaa ya Kanyenye, Uswetu na Maili tano zenye thamani ya bilioni 16.4 ambayo ilibainika kucheleweshwa.

Ameeleza kuwa miradi hii ilitakiwa kukamilika Februari 19, 2025 lakini hadi kufikia Machi 2025, utekelezwaji wake ulikuwa chini ya asilimia 61 na kubainisha uwezo mdogo wa taasisi hizo kuwa ndio sababu ya kuchelewa. 

Aidha taasisi hiyo imebaini kuwepo kwa mwingiliano wa miundombinu ya maji inayomilikiwa na TUWASA inayopita kwenye barabara hivyo akashauri kuwepo njia mbadala za kupitisha miundombinu ya maji wakati wa utekelezaji miradi hiyo.