November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Mkoa wa Tanga yawabaini watumishi wa afya waliosajili wagonjwa hewa wa VVU

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru Mkoa wa Tanga imewabaini watumishi wa afya katika wilaya ya Muheza waliohusika kusajili wagonjwa hewa 313 wa virusi vya Ukimwi (VVU) ili kuonyesha takwimu zipo juu za wanaoishi na VVU kwa maslahi yao binafsi ikiwemo kujinufaisha na fedha zinazotolewa na shirika la afya la AMREF.

Fedha hizo zinalipwa na Shirika hilo la afya la (AMREF) kama motisha kwa watumishi hao, zimepelekea watoa huduma hao kuongeza idadi ili waweze kujipatia fedha hizo.

Fedha hizo hulipwa moja kwa moja kwa muhudumu wa afya kupitia akaunti yake ya simu kwajili ya kazi ya kufuatilia kila mgonjwa kwa lengo kuhakikisha hali yake ya kiafya inaimarika kwa maana ya kutumia dawa kwa wakati na huduma nyingine zinazostahili.

Ufuatiliaji wa takwimu Mkoa wa Tanga umebaini kuwa wahudumu wa afya wanaohusika na zoezi la kuwasajili na kuwafuatilia wagonjwa wanaoishi na VVU wamekuwa wakilipwa posho ya gharama ya usafiri na mawasiliano kiasi cha shilingi elfu 20,000 kila wanapotoka kwenda kuwatembelea wagonjwa hao fedha zinazolipwa na shirika la afya AMREF.

Awali akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Takukuru Mkoa Tanga Zainabu Bakari amesema walibaini udanganyifu huo baada ya uchunguzi na kugundua watoa huduma za Afya wilayani Muheza wanahusika na kusajili majina hewa ya wagonjwa wa Virusi vya Ukimwi ili kuzidisha takwimu za ugonjwa huo kwa maslahi yao binafsi.

Alisema wahudumu wa afya wanaohusika na zoezi la kusajili na kuwafuatilia watu wanaoishi na VVU wilayani humo, wamekuwa wakilipwa posho ya gharama ya usafiri na mawasiliano kiasi cha sh. 20,000 kwa siku kila wanapowatembelea wagonja hao.

“Katika kipindi cha kunzia Julai hadi Septemba mwaka huu Takukuru imefanikiwa kudhibiti jumla ya wagonjwa hewa 313 wa VVU kwenye mfumo wa usajili wa wagonjwa wilayani Muheza,” alisema Kamanda huyo.

Aidha amesema idadi hiyo ya wagonjwa iliondolewa kwenye mifumo na wahusika waliohusika na usajili wa wagonjwa hewa walipewa barua na kujieleza kwa kitendo cha kusajili wagonjwa hewa ambapo Wizara ya afya imetoa maelekezo ya kufanya ihakiki kwa wateja wanaotumia dawa ambao sio halisi.

“Kitengo hicho cha muhudumu kupewa fedha hiyo moja kwa moja katika akaunti yake ya simu au simu yake ya mkononi ndicho kilichopelekea watumishi wasiokuwa waadifu kutumia nafasi yao vibaya na baada ya kubainika kitu hicho tulifanya udhibiti wa jambo hilo, “alisistiza Mkuu huyo wa Takukuru.

Aidha Takukuru ilitembelea Zahanati 7 kati ya 16 zilizopo katika wilaya ya Muheza na kubaini tatizo hilo hivyo Takukuru imemuagiza Mganga mkuu wa wilaya hiyo kufanya uhakiki wa tawkimu za wagonjwa wote wanaoishi na VVU na kuwapatia taarifa hizo za uhakiki.

Kamanda huyo alisema baada ya kubaini suala hilo waliandaa kikao cha pamoja katia yao na ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya hiyo na wahusika wote wa takwimu hizo, na kuagiza kufanywa upya wa uhakiki wa majina ya wagonjwa hao.

Watumishi waliohusika ambao hawakutajwa idadi yao, tayari wamepewa barua za kiutumishi ili wajieleze kabla ya hatua kuchukuliwa dhidi yao.

Katika hatua nyingine kamanda huyo amesema kuwa Takukuru imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Chama Cha skauti (TAKUSKA) kwa lengo la kuwafundisha vijana katika mapambano ya kuzuia rushwa ili wawe ni sehemu mojawapo katika kuunga mkono juhudi za kukomesha vitendo vya rushwa kwenye jamii.

” Uelimishaji ni mwendelezo wa utekelezaji wa mpango kazi wa ushirikiano Kati ya Takukuru na skauti uliowekwa kwa lengo la kuwafundisha vijana wa skauti kuhusu kuzuia na kupambana na rushwa nchini ili wawe ni sehemu ya jamii inayotekeleza jukumu la ufwatiliaji wa matumizi ya rasilimali za Umma” alisema.

Aliongeza kuwa kupitia Takukuru inayotembea wamejiwekea utaratibu wa kuwafikia wananchi kuelimisha juu ya madhara yatokanayo na kujihusiaha na vitendo vya rushwa huku akiwataka kuendelea kutoa taarifa Mara tu wanapobainishi viashiria vya rushwa katika maeno yao.