December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU kuwafikisha 8 mahakamani kwa tuhuma za rushwa

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online,Dodoma

TASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya mashtaka leo inawafikisha mahakamani watuhumiwa wanane kwa tuhuma za rushwa, uhujumu uchumi pamoja na wizi wa kiasi cha zaidi ya shilingi billion nane ambazo ni mali ya mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Kati ya watuhumiwa hao, saba walikuwa ni wafanyakazi wa TPA ambao hivi sasa wameshafukuzwa kazi kwa mujibu wa sharia, na kati ya hao mmoja wao ni wakili wa kujitegemea.

Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na TAKUKURU Makao Makuu na kusainiwa na Afisa wa Habari, Doreen Kapwani watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni pamoja na  aliyekuwa Mhasibu Mwandamizi Deogratius Lema, aliyekuwa Afisa Uhasibu Aike Mapuli wote kutoka TPA Makao Makuu, aliyekuwa Afisa Uhasibu TPA Marystelle Minja na aliyekuwa Mhasibu wa kituo cha Bandari Mwanza Thomas Akile.

Wengine ni aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Kituo cha Bandari Mwanza Ibrahim Lusato, aliyekuwa keshia wa Kituo cha Bandari Mwanza Wendelini Tibuhwa, aliyekuwa Afisa Kodi wa Kituo cha Bandari, James Mbedule na Wakili wa Kujitegemea Leocard Wilfred.

Taarifa hiyo imesema kuwa uchunguzi umebaini watuhumiwa hawa kwa pamoja wamehusika kutenda makossa ya uhujumu uchumi na rushwa yakiwemo kula njama kwa kutenda kosa, kughushi, kuunda genge la uhalifu, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuisababishia mamlaka hasara na utakatishaji wa fedha haramu na kusababisha upotevu wa fedha zaidi ya shilingi billion nane.

Adha taarifa hiyo inasema pamoja na kufikishwa mahakamani bado uchunguzi wa Takukuru unaendelea kwa ajili ya kubaini kiasi cha fedha nyingine ambazo zimehujumiwa ikiwemo kuwatafuta wahalifu na kuchukua hatua za kisheria kwa watuhumiwa wengine ambao wamehusika ili waweze kuunganishwa katika shauri hilo.