Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imebaini wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi mkoani humo wamezidiwa na uhitaji mkubwa wa vifaa hivyo katika ujenzi wa miradi ya maendeleo jambo ambalo linakwamisha miradi hiyo kukamilika kwa waka
Hayo yameelezwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Faustine Maijo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi ya kipindi cha robo ya pili ya mwaka kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba, 2023 ambapo taasisi hiyo imefanikiwa kufuatilia utekelizaji wa miradi 11 yenye thamani ya bilioni 9.57.
Maijo ameeleza kuwa taasisi hiyo imebaini ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi ambavyo vinatakiwa kupelekwa katika maeneo ya miradi akitolea mfano kusuasua kwa ujenzi mkubwa wa shule ya sekondari ya wasichana ya bweni yenye thamani ya bilioni 3 katika Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda ni vifaa kushindwa kufika kwa wakati.
“Ucheleweshaji wa vifaa umekuwa changamoto kubwa kuna kipindi ni kama Mkoa wetu ulizidiwa,usabazaji wa vifaa vya ujenzi ukawa hauendi kwa wakati lakini wakati mwingine ni uzembe wa wasimamizi kushindwa kufanya taratibu za manunuzi,”amesema Maijo.
Amefafanua kuwa kuzidiwa kwa wasabazaji ni kwa sababu serikali imeleta fedha nyingi za miradi mingi katika Mkoa wa Katavi na kuhitajika kutekelezwa kwa wakati mmoja.
Pia amesema kuwa jitihada wanazofanya kwa sasa ni kuhamasisha wafanyabiashara waweze kuongezeka na kuleta mzingo mkubwa wa vifaa vya ujenzi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili panapokuwa na uhitaji mkubwa wa vifaa hivyo vipatikane kwa haraka.
“Takukuru itafanya vikao na wafanyabiashara kupitia mpango wake wa TAKUKURU RAFIKI na kuwaeleza kwamba kuna maeneo tunakosa huduma ya vifaa vya ujenzi hivyo walete kwa wingi ili kuhakikisha miradi inayojengwa isikwame” Amesema.
Changamoto nyingine inayokwamisha miradi kukamilika ni kutofuata taratibu za manunuzi,wizi wa saruji na vifaa vingine vya ujenzi,usimamizi usio bora wa miradi na kutoroka kwa mafundi kipindi cha kilimo ambapo taasisi hiyo inayafuatilia na kuchukua hatua za kisheria.
Amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa TAKUKURU ili waweze kudhibiti mianya yote ya rushwa na kwa watumishi na watu wote ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa waweze kubainishwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu na sheria.
Zawadi Maganga,Mkazi wa mtaa wa Misukumilo Manispaa ya Mpanda licha ya kuipongeza TAKUKURU amesema kuwa serikali ya Mkoa wa Katavi inajukumu kubwa la kuhamasisha wafanyabiashara kufungua maduka mengi ya vifaa vya ujenzi ili kukuza ushindani kwenye soko la biashara.
Ameomba serikali kushawishi wawekezaji wa kujenga viwanda katika mkoa huo jambo ambalo litachangia sio bei ya vifaa vya ujenzi pekee kushuka bali upatikanaji wa vifaa hivyo kutosheleza mahitaji ya ujenzi mbalimbali ya miradi ya maendeleo.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote