December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Igunga yawafikisha mahakamani Polisi sita kwa tuhuma za rushwa

Na Allan Vicent, TimesMajira,Online Igunga.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Igunga Mkoani Tabora imewafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga askari polisi sita na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Isakamaliwa kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya sh. mil 8.4 kutoka kwa wazee wawili wa kijiji cha Isakamaliwa akiwemo mzee wa miaka 85. Mwendesha Mashtaka wa Taasisi hiyo wilayani hapa, Mazengo Joseph ametaja majina ya askari hao kuwa ni Inspekta Msaidizi, Frank Matiku (36), PC. Raphael Charles (31), Koplo Paul Bushishi (49), PC Lucas Nyoni (31), PC Lome Laizer (39) Koplo Charles Zacharia (45) na Ofisa Mtendaji wa kijiji Edward Kitenya (42).

Mazengo ameiambia mahakama kuwa washtakiwa wote 7 walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha sheria ya TAKUKURU Na. 11 ya mwaka 2007.

Akisoma mashitaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa wilaya hiyo, Eddah Kahindi, amesema kuwa washtakiwa wote saba wanakabiliwa na mashitaka manne.

Ametaja mashtaka hayo kuwa ni kuomba rushwa ya sh. mil. 8 kutoka kwa Mzee Nkende Ngaka Mataluma mkazi wa kijij cha Isakamaliwa, ambapo Juni 12, 2019 muda wa saa 4 asubuhi walifika katika kijiji hicho na kuomba kiasi hicho ili wasimchukulie hatua baba yake, Ngaka Mataluma ambaye walimtuhumu kujihusisha na tiba asili bila kibali ikiwemo kukutwa na silaha kinyume na utaratibu.

Shtaka la pili ni kupokea rushwa ya sh. mil. 8 kutoka kwa Mzee Nkende Ngaka na mwenzake, Maulid Hamisi Kapila kama kishawishi ili wasiwachukulie hatua ya kisheria baba yao, Ngaka Mataluma Fale.

Shitaka la tatu alisema kuwa ni kuomba rushwa ya sh. 450,000 kutoka kwa Jilumba Hamka Habi katika tarehe hiyo hiyo na mwezi huo ambapo washtakiwa hao waliomba kiasi hicho cha fedha ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa kukutwa na nyara za serikali.

Mwendesha mashtaka huyo ameongeza kuwa shtaka la nne ni kupokea rushwa ya sh. 450,000 kutoka kwa Mahega Sali ambaye ni mtoto wa Jilumba Hamka Habi ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa kukutwa na nyara za serikali.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yao walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashtaka ulidai upelelezi umekamilika na kesi hiyo itaanza kusikilizwa April 17 na 18, 2021. Washtakiwa wako nje kwa dhamana ya sh mil. 8 kila mmoja.