September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU: Hatuhusiki kubambikia watu kesi utakatishaji, uhujumu uchumi

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

TAASISI ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu Brigedia Jenerali John Mbung’o, imekanusha kuhusika kuwabambikizia wananchi kesi za tuhuma za rushwa, utakatishaji fedha na kuwataifishia fedha za watuhumiwa hao katika akaunti zao za benki.

Brigedia Mbung’o amesema kuwa, taarifa hizo ambazo zimekuwa zikisambaa katika mitaondao si za kweli kwani zina nia ovu ya kujenga chuki dhidi ya wananchi kwa Serikali yao.

Amesema, TAKUKURU inapokuwa imepokea tuhuma, inafanya uchunguzi ili kupata ushahidi na mara baada ya kukamilisha upatikanaji wa ushahidi huo, jalada hupelekwa kwa Mkurugenzi wa mashitaka ya umma (DPP) kwa ajili ya mapitio ya ushahidi uliokusanywa.

“DPP akiridhika na ushahidi huo kwenye jalada la uchunguzi ndipo kesi inafunguliwa mahakamani, huu ndio mchakato ambao hatuoni ni kwa namna gani suala la kubambikiziwa kesi litakavyojitokeza, ” amesema na kuongeza.

“Wananchi wa Tanzania wanalindwa na Katiba ya nchi na ndio maana wanapotuhumiwa kwa makosa yoyote yakiwemo ya rushwa watuhumiwa hao huwa na haki ya kujitetea ikiwa ni pamoja na kuwa na mawakili,” amesema Mkurugenzi huyo.