Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online, Mbeya
Kufuatia utekelezaji wa taratibu za utoaji wa mbolea za ruzuku tayari wakulima 500 wa Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wamesajiliwa ili kunufaika na ruzuku ya mbolea itakayotolewa msimu ujao wa kilimo.
Hayo yalibainika wakati wa ziara ya watendaji wa Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walipotembelea wilaya hiyo ili kujionea mwenendo mzima wa usajili wa wakulima.
Akizungumza katika vituo mbalimbali vilivyokuwa vikisajili wakulima Meneja Uagizaji na uuzaji mbolea nje ya Nchi, Louis Kasera aliwataka wakulima waliosajiliwa kuwa mabalozi kwa wakulima wengine ili wafike kujisajili.
“Hakuna mbolea ya ruzuku pasipo kusajiliwa” alikazia Kasera na kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili wakulima umeanza mapema ili ufikapo msimu kilimo wakulima waweze kupatabidhaa hiyo kwa wakati.
Kwa upande wake, Afisa Biashara Mwandamizi, Doto Detteba, alisema ukusanyaji wa taarifa za idadi ya wakulima na ukubwa wa mashamba wanayoyamiliki zitaisaidia serikali kujua idadi ya wakulima wanaopatikana katika eneo hilo na kiasi cha mbolea kitakachohitajika kulingana na ukubwa wa mashamba yanayomilikiwa na wakulima wa eneo husika.
Ameongeza kuwa ni sharti shamba moja limilikiwe na mtu mmoja na si kila mwanafamilia kujisajili kwa kutoa taarifa za shamba moja.
Kwa upande wake, Elius Mtware Mjumbe halmashauri ya kijiji cha Godima Wilayani Chunya ameishukuru serikali kwa kwawakumbuka wananchi kutokana na hali duni walizonazo utoaji wa mbolea za ruzuku utawasaidia kuzalisha kwa tija.
Aidha ameiomba serikali kutoa msaada kupata ruzuku hata kwa pembejeo nyingine za kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao wanayolima.
Usajili wa wakulima ni moja ya mikakati ya kudhibiti utoaji wa mbolea za ruzuku kwa mwaka huu wa fedha ili kuhakikisha wakulima halisi wananufaika na mbolea za ruzuku na kusababisha uwepo wa chakula nchini.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote