Na David John,TimesMajira Online, Dar
SHIRIKA la Health and Wealth(TAHA)imewakikishia Watanzania kwamba inaendelea kufanya kazi ya kuimarisha tasnia ya kilimo cha horticulture kwa kuunganisha na kuratibu wahusika wa mnyonyoro wa thamani katika kilimo.
Lengo la TAHA ni kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo cha horticulture hapa nchini kwa ukuaji jumuishi hai na endelevu na kwamba TAHA ni asasi ama sekta binafsi ambayo inatetea ukuaji na ushindani wa sekta ya kilimo nchini tangu ilipoazishwa mwaka 2004.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa leo yanayoendelea mkoani Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano kwa Wateja wa Shirika hilo Lovennes Adolf amesema wamekuwa jukwaa la kutoa sauti kwa wazalishaji, wafanyabiashara, wauzaji bidhaa pamoja na wasindikaji wa mazao ya horticulture kama maua, matunda , mbogamboga, mimea tiba, viungo na mazao yatokanayo na mimea.
Ameongeza kuwa “Shirika linalinda masilahi ya sekta binafsi na kuhakikisha masuala ya sekta ya kilimo cha maua yanajumuishwa vizuri katika ajenda za kitaifa, kikanda na kimataifa,na inatekeleza shughuli zake za kibiashara ili kufikia malengo yake kwa kukuza na kuhuisha uzoefu katika sekta hiyo.
Amesema dira shirika ni kuwa sekta mahiri ya uchumi, mafanikio endelevu ya tasnia ya horticulture wakati dhima yao ni kusimamia ukuaji jumuishi, mabadiliko , ushindani na maendeleo ya sekta ya kilimo Tanzania.
Ameongeza kuwa katika kutekeleza dira na dhamira yao TAHA kwa kushirikiana na wadau wanaongozwa na madili sita uwazi, heshima kwa wote, uwajibikaji, kujali wateja, kuzingatia muda na wakati pamoja na uendelezaji na ujumuishaji.
Akizungumzia maonyesho hayo Adolf amesema wanatambua umuhimu wa maonesho na ushiriki wao umesaidia kukutana na wananchi mbalimbali ambao wamekuwa wakifika kufahamu shughuli za TAHA.
Amefafanua kuwa matumaini yao kama TAHA baada ya kumalizika kwa maonesho hayo watakuwa wamepata mabalozi wazuri ambao watakuwa mstari wa mbele kulizungumzia Shirika hilo.
Pia amesema TAHA inaendesha kazi zake kwenye mikoa 25 Tanzania Bara na Visiwani ikiwamo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga,Dodoma,Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya , Pwani, Dar es Salaam , Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Shinyanga, Singida , Songwe, Unguja Mjini/Magharibi, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja,Kusini Pemba na Kaskazini Pemba.
“Ndugu zangu wanahabari TAHA tunatekeleza shughuli zetu kupitia mfumo wa kongani kama sehemu ya kufikia jamii ambazo zimelengwa kikamilifu hivi sasa,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mazingira wezeshi ya biashara TAHA huainisha na kuchambua sera, kanuni na sheria zinazohusu kilimo na biashara ya mazao ya horticulture na kuishauri Serikali namna bora ya kuziboresha.
“TAHA imefanikiwa kuishawishi Serikali kufanya mabadiliko mbalimbali ya kisera, kikanuni na kisheria kwa lengo la kuboresha mazingira wezeshi ya biashara nchini.”
Amesema miaka ya nyuma walikuwa wanashirikiana na kampuni nyingine ambao ni watoa huduma na wanachama wa TAHA ambao wamekuwa wakitumia maonesho hayo kuonesha bidhaa zao kama mbegu, dawa na mbolea lakini mwaka huu wameona watoe nafasi kwa wajasiriamali wadogo ambao wanasindika bidhaa mbalimbali.
Ameongeza wajasiriamali ambao wamekuwa nao mwaka huu katika maonesho hayo ya biashara ya kimataifa wanatoka Tanzania Bara na Visiwani.”Katika banda letu mwaka huu tunao wajasiriamali 10 ambao wamekuja na bidhaa tofauti zikiwemo viungo pamoja na matunda ambayo wameyachakata kwa ajili ya matumizi.
“Kwa hiyo ni fursa kwao na tunategemea kupitia maonesho haya watakuwa wamejitangaza na kuweza kupata biashara nyingi zaidi, na tunatarajia watatupa mrejesho huko wanakokwenda kuhusu biashara zao.
“Wanaokuja banda la TAHA wanataka kujua tuko kwenye mikoa gani na huduma gani ambazo tunazitoa, kimsingi wanaokuja hapa sio kwamba ndio mara ya kwanza wanatuona bali wameshatusikia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kwa sasa dunia ni kama kijiji,” amesema.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi