Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora
KANISA la Tanzania Assemblies of God (TAG)-Kitete Christian Centre (KCC) lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,limesema kuwa amani na utulivu uliopo nchini ni matokeo ya uongozi mzuri wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Hivyo ametoa wito kwa waumini wa kanisa hilo na jamii kwa ujumla kuendelea kumwombea ili Mungu aendelee kumwongoza huku limempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utendaji mzuri na mafanikio yaliyopatikana.
Pongezi hizo zimetolewa Desemba 25,2024 na viongozi wa kanisa hilo kwenye ibada ya sikukuu ya Krismas ambapo walieleza kufurahishwa na amani kudumishwa na utulivu wa Watanzania.
Askofu Mstaafu na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Rev.Paul Meivukie,amesema kuwa Watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuwapa Rais mchapakazi, asiye na makuu na anayejali ustawi wa wananchi wake.
‘Kupitia ibada hii naomba Mungu ampe afya njema, uzima na maono makubwa ya kuwatumikia watanzania ili kuharakisha kasi ya maendeleo yao, pia amani na utulivu viendelee kutamalaki hapa nchini’, amehitimisha.
Mchungaji Msaidizi wa Kanisa hilo Zakaria Stephano,amebainisha kuwa tunapoadhimisha sikukuu hii ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, waamini wote na wasio waamini wanapaswa kumshukuru Mungu kwa mambo makubwa yaliyofanyika hapa nchini.
Mzee wa Kanisa hilo ambaye pia ni Katibu wa Kanisa, Mathias Chivinja,amebainisha kuwa utendaji wa Rais Samia umesaidia kupunguza vitendo vya utekaji wananchi ikiwemo kukamatwa baadhi yao, ameomba waumini wa kanisa hilo kuendelea kumwombea ili Mungu amwongoze katika utumishi wake.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake