January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAFU yaomba kuanzishwa Wizara ya Ujasiriamali na Ukuzaji Mitaji

Judith Ferdinand, Mwanza


Chama cha Wavuvi Tanzania (TAFU),kimetoa ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuanzisha Wizara ya Ujasiriamali na Ukuzaji Mitaji ambayo itajikita kuwasaidia wajasiriamali(wafanyabiashara wadogo), kukua katika biashara zao.

Hali itakayosaidia kujenga uchumi katika kuelekea uchumi wa blue na wa kati ambao taifa limekuwa likitamani kuona wananchi wake wanafikia huko.

Ombi hilo limetolewa na Msemaji wa Chama cha Wavuvi Tanzania (TAFU),Sijaona James,wakati akizungumza na Majira mara baaada ya kumalizika kwa kikao cha wadau wa Mwanza kwa ajili ya kupokea maoni kwenye mapitio ya sera ya taifa ya taifa ya mwaka 2003, kilichofanyika mkoani Mwanza.

Kikao hicho kilichowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali mkoani Mwanza kiliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Sijaona amesema,unapozungumza biashara,unazungumzia biashara inayo kua na inayo endelea,hivyo hauwezi kuwa na biashara hizo kama hauna msingi wa wafanyabiashara wadogo ambapo wanapozungumzia wafanyabiashara leo hapa nchini asilimia 80 ni machinga/wajasiriamali.

Amesema,kama taifa halina sera ya kukuza mitaji na kusaidia wafanyabiashara wadogo kukua kibiashara katika nchi haiwezi kupata mabilionea wala kupata wafanyabiashara wa kati.

Hivyo mkakati wa kuwasaidia wafanyabiashara wadogo katika nchi na kuwa na sera ya biashara ambayo itasaidia kukuza biashara na kusaidia mitaji katika kukuza biashara itasaidia kupata mabilionea.

“Ndio maana mimi leo nimetumia fursa hii kushauri,salamu zimfikie Rais wa Jamhuri ya Tanzania kuwa moja ya mchango mkubwa ni kutengeneza Wizara ya Ujasiriamali na Ukuzaji mitaji hii isaidie kuwapa elimu,kuwapa mitaji na kuwaongoza wafanyabiashara wadogo,”amesema Sijaona na kuongeza kuwa

“Pia kuwe na Wizara ya Matumizi ambayo itasaidia nchi kukua,hivyo kuwe na sera ya kulinda mitaji ili kupata wafanyabiashara watakaoweza kwenda kushindana katika masoko ya nje ikiwemo la Afrika Mashariki,”.

Sanjari na hayo amesema,wanaona sera zao zinakosa tija kwa sababu ya changamoto nyingi za kikanuni na kisheria kwani ata kukiwa na sera nzuri lakini kama hakuna kanuni na sheria nzuri haitosaidia.

Hivyo sera hii lazima iendane na mabadiliko makubwa ya sheria za nchi pamoja na kanuni kwenye idara mbalimbali ambazo zitawezesha watu kufanya biashara.

“Sisi tunashauri,mfano katika kikao cha leo Mwanza tunaamini mawazo yote yaliyotolewa katika kikao hichi ndio mawazo ya wafanyabiashara halisi,tunategemea mawazo yote watayaweka katika sera hiyo na kuweza kuboreshwa ili kuwe na sera yenye tija,”.

Kwa upande wake Ofisa Habari na Mawasiliano ya Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL)Edmond Rutajama amesema kuna sera ya taifa ya biashara na sera ya masoko ya mazao ya kilimo inayowagusa wao ambapo kimsingi serikali inatoa fedha nyingi kwenye meli zao mfano hapa Mwanza kuna meli ya New Victoria hapa kazi tu ambayo inafanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba.

Hivyo wateja wao wakubwa ni wasafirishaji wa mizigo ambao ni wafanyabiashara,miaka mitatu nyuma serikali ilielekeza kuwa kwa mkulima mzigo wowote chini ya tani asitozwe tozo yoyote.

Lakini kumekuwa na changamoto ya Halmashauri ya Jiji kuwa na tozo nje ya uzio wa bandari ambapo wameweka beria wakiwasumbua wafanya biashara wakati serikali ilielekeza Halmashauri, Manispaa na majiji tasitoze ushuru wa kutoka halmashauri moja kwenda nyingine.

“Sasa nashukuru mmekuja mtusaidie kwa hili kwani mfanyabiashara huyo nje ya bandari anatozwa ushuru na Halmashauri ya Jiji na akiingia ndani ya bandari anatoa tozo ya bandari kwaio tozo zinakuwa nyingi na kufanya wateja kutukimbia,kwani dugu zetu wakulima ndio wanasafirisha ndizi na mazao mengi kutoka kagera kuja Mwanza Mwanza kagera na kwingineko kwa kutumia meli yetu,”amesema Rutajama.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara,Alfred Mapunda,amesema
utungaji wa sera lazima ushirikishe wadau ambapo wadau wa Mwanza ni baadhi ya wadau ambao wanaenda kuwapitia ikiwemo Kagera na maeneo mengine.

Amesema, unapo pokea mawazo ya wadau wakati mwingine yanakinzana,hivyo sera unayoitunga lazima uhakikishe haikizani lakini mawazo ya wadau lazima yazingatiwe kwa sababu wao ndio wenye sera hiyo.

Msemaji wa Chama cha Wavuvi Tanzania (TAFU), Sijaona James, akizungumza na Majira mara baada ya kumalizika kwa kikao cha wadau wa Mwanza kwa ajili ya kupokea maoni kwenye mapitio ya sera ya taifa ya biashara ya mwaka 2003, kilichofanyika mkoani Mwanza,ambacho kiliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.picha na Judith Ferdinand
Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau wa Mwanza kwa ajili ya kupokea maoni kwenye mapitio ya sera ya taifa ya biashara ya mwaka 2003, kilichofanyika mkoani Mwanza,ambacho kiliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.picha na Judith Ferdinand
Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Alfred Mapunda akizungumza na waandishi mara baada ya kumalizika kwa kikao cha wadau wa Mwanza kwa ajili ya kupokea maoni kwenye mapitio ya sera ya taifa ya biashara ya mwaka 2003, kilichofanyika mkoani Mwanza,ambacho kiliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.picha na Judith Ferdinand