Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imekubaliana kimkakati na kampuni binafsi inayojishughulisha na kilimo ya Private Agricultural Sector Support (PASS Trust) yanayolenga kuwawezesha vijana na wanawake kupata mikopo itakayoinua shughuli zao za kilimo hapa nchini.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kufanya mazungumzo, Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust, Johane Kaduma, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege alisema makubaliano ya taasisi hizo mbili yanalenga kuwawezesha vijana na wanawake ili waweze kunufaika na mikopo moja kwa moja sambamba na kuchangia maendeleo ya ukuaji wa sekta ya kilimo.
“TADB na wenzetu wa PASS Trust wote tumekuwa tunajishughulisha na kuinua sekta ya kilimo, hivyo kutokana na umuhimu huo tumekubaliano kuongeza nguvu na hasa kwa vijana ambao ndio nguvu kazi kwa taifa na wanawake ambao sehemu kubwa wamekuwa wakijishughulisha na kilimo waweze kupata mikopo nafuu itakayo wanufaisha kuendesha shughuli za kilimo chenye tija”, alisema Nyabundege.
Aliongeza kuwa benki yake itaendeleza jitihada zake za kuhakikisha kuwa inatoa mchango katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ilikuchochea maendeleo ya ujenzi wa viwanda hapa nchini.
“Makubaliano yetu ni sehemu ya mipango mikakati ya TADB ya kutengeneza mazingira bora ya wakulima kunufaika na mikopo nafuu na pia nachua fursa hii kuwaomba wakulima hapa nchini katika makundi haya mawili muhimu ya wanawake na vijana kuchangamkia fursa kama hizi zinapojitokeza,” alisema.
Aidha, Nyabundege alisema ushirikiano wao unalenga pia sio tu kuwajengea uwezo wa ujuzi vijana bali kuwapatia mitaji ambayo itaenda kufungua njia/mbinu ya kujiajiri kwa idadi kubwa ya vijana.
Kwa upande wake, Kaduma aliishukuru na kuipongeza TADB kwa jitihada wanazozifanya katika kuleta mageuzi ya katika sekta ya kilimo na kueleza kuwa taasisi yake inajivunia kuingia ubia na benki hiyo ambayo utawafungulia fursa vijana kuweza kujiajiri kupitia mikopo.
“Kwa mujibu wa Shirika la kimataifa la Kazi Duniani (ILO) ukosefu wa ajira unakadiriwa kuwa asilimia 13.4 kwa vijana wenye umri wa miaka 15 mpaka 34 huku, hivyo basi imani yangu ni kuona vijana hawa wakinufaika na ubia huu ili kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira nchini,” alisema Kaduma.
Alieleza kuwa, “Ubia huu umefikiwa wakati muafaka kwani malengo yake yanayosadifu matarajio ya Serikali ya awamu ya sita ya kuona sekta ya kilimo inatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kuchochea ongezeko la ajira.
Ubia huo wa TADB na PASS TRUST unatarajiwa kuleta matokeo chanya na kuinua sekta ya kilimo ambayo imeajiri watanzania zaidi ya asilimia 65%. TADB imeendelea kupongezwa sehemu mbalimbali nchini kwa mchango wake.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato